Mizozo na migogoro imeongezeka ndani ya utawala wa Kizayuni kiasi kwamba, rais wa utawala huo pandikizi, Isaac Herzog ametishia tena kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe na hali ya Israel kuripuka kutokana na mizozo ya kisiasa na mifarakano shadidi katika jamii ya utawala wa Kizayuni.
Baraza jipya la mawaziri la Benjamin Netanyahu ambalo ni baraza lake la sita tangu mwaka 1996 lilipasishwa na bunge la Israel tarehe 29 mwezi uliopita wa Disemba, 2022. Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, serikali hiyo imekumbwa na matukio machungu yanayotishia kuisambaratisha na kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya utawala wa Kizayuni.
Kabla ya hapo pia na kutokana na kuzuka mzozo wa kisiasa kati ya makundi ya Israel, bunge la utawala huo lilivunjwa na serikali nayo ilisambaratika. Wasiwasi wa kujikariri jambo hilo kwa mara ya nne mfululizo umezusha wasiwasi wa kutokea mkwamo mkubwa wa kisiasa ndani ya utawala huo dhalimu. Lakini kinachoonekana wazi zaidi hivi sasa ni hatari ya kutokea vita vya ndani baina ya Wazayuni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana rais wa utawala huo, Isaac Herzog akasema: “Mimi ninaona kambi ambazo zinaelekea upande wa vita vikubwa. Nina wasiwasi kwamba tumekaribia kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na huenda vita hivyo vikatuangamiza kabisa.” Hii si mara ya kwanza kwa Herzog kutamka maneno kama hayo ya hatari ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya utawala wa Kizayuni katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.
Amma swali muhimu zaidi linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kitu gani kimefanya rais wa utawala wa Kizayuni azungumzie hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Israel kwa mara kadhaa sasa?
Wachambuzi wa mambo wanasema, huenda ni sababu mbili zifuatazo ndizo zilizomfanya Isaac Herzog atoe maonyo ya mara kwa mara ya kutokea vita hivyo vya ndani huko Israel. Sababu ya kwanza ni muundo wa serikali ya Benjamin Netanyahu. Kituo kimoja cha utafiti cha Kiarabu kimeandika: Baraza la sita la mwaziri la Netanyahu ndilo baraza lenye misimamo mikali zaidi katika historia ya Israel kwani baraza hilo linajumuisha vyama vya kifashisti vyenye misimamo ya kuchupa mipaka vya mrengo wa kulia tena katika pande zote mbili, upande wa wasiojihusisha na dini na upande wa wanaojihusisha na dini. Hii ina maana kwamba chama cha Likud ambacho katika miaka ya hivi karibuni kimechochea mno misimamo mikali na ya kibaguzi, kimeungana na vyama viwili vyenye misimamo mikali ya watu wanaojihusisha na dini na wale wasiopenda dini, na kuunda serikali chini ya muungano wa vyama hivyo vitatu vya kifashisti.
Muundo wa serikali mpya ya utawala wa Kizayuni ni wa namna ambayo iwapo kutatokea mkwamo wa kisiasa, basi Israel itatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Watu kama Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni ndio watakaozusha vita hivyo ndani ya Israel. Ni kwa sababu hiyo ndio maana hivi sasa wahka umetanda katika anga ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Naam, kuna hatari ya kusambaratika serikali mpya ya Netanyahu na kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya utawala huo wa Kizayuni.
Sababu ya pili muhimu inayomfanya rais wa utawala wa Kizayuni, Isaac Herzog, kutoa maonyo ya mara kwa mara ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenye ndani ya utawala huo pandikizi, ni kwamba jamii yenyewe ya Israel kwa miaka mingi sasa imekumbwa na mizozo kiasi kwamba kuna mizozo mikubwa baina ya Waarabu na Mayahudi bali hata vita baina ya pande hizo mbili vimetokea kwenye kipindi cha hivi karibuni na kusababisha vifo na majeruhi. Ubaguzi wa kizazi ni mkubwa ndani ya utawala wa Kizayuni kiasi kwamba Jumanne wiki hii, bunge la utawala huo dhalimu lilirefusha muda wa sheria ya kibaguzi ambayo wahanga wake wakubwa ni Waarabu wanaoishi kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Wachambuzi wa mambo wa Kipalestina wanasema kuwa, hizo zote ni njama za Israel za kuufuta utawala wa ndani wa Palestina na kuziingiza ardhi za Ukingo wa Magharibi ndani ya ardhi nyingine za Palestina zikazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni tangu mwaka 1948.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana rais wa Israel, Isaac Herzog, akasema wakati huu ambapo imebakia miaka mitano hadi kufikia miaka 80 ya kuasisiwa utawala pandikizi wa Israel huko Palestina, kwamba kuna haja kwa Wazayuni kuweka pembeni mizozo yao, vinginevyo kutazuka vita vya ndani baina yao na kuwaangamiza wote.