Onyo la Katibu Mkuu wa UN la kutokea vita vya nyuklia duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani. Alitoa onyo hilo Jumatatu, Agosti 1, 2022 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kuangaliwa Upya Mkataba wa NPT wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, António Guterres alisema, uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia duniani haujawahi kuwa mkubwa kiasi hiki tangu vilipomalizika vita baridi na kwamba kosa moja tu la kimahesabu linaweza kuutumbukiza ulimwengu kwenye janga la vita vya nyuklia lisilolipizika. Infaa kuashiria hapa kwamba mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika tangu mwaka 2020 lakini ulikuwa ukiakhirishwa mara kwa mara kutokana na janga la UVIKO-19 yaani corona.

António Guterres pia amesema, hadi kufikia hapa tulipofikia, sisi tunahisi tumekuwa na bahati sana lakini bahati si kitu cha kukitegemea muda wote. Kutegemea bahati kamwe haiwezi kuwa njia ya sahihi ya kuzuia kutokea vita vya nyuklia. Njia pekee ya kuzuia vita kama hivyo ni kuangamizwa silaha zote za nyuklia duniani, amesema kwa kusisitiza.

Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: Hivi sasa kuna takriban silaha 13,000 za nyuklia katika maghala ya silaha ya maeneo tofauti duniani. Silaha hizo zinaongezeka kila kukicha huku vizuizi vya kuzuia kutokea vita na ugomvi vikizidi kupungua siku baada ya siku.

Ni uhakika usiopingika kwamba kuongezka maghala ya silaha za nyuklia duniani na ushindani mkubwa uliopo baina ya mataifa yanayomiliki silaha hizo haramu ambayo yanazidi kufanya juhudi za kuwa na silaha kali zaidi za atomiki, ni mambo ambayo yameuweka usalama wa dunia katika hatari kubwa. Kwa kweli onyo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa linapaswa kutiliwa maanani sana hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote kutokana na kuongezeka vibaya makabiliano baina ya Russia na Marekani katika kadhia ya vita vya Ukraine na hasa baada ya Moscow kuonesha mabavu yake ya nguvu za nyuklia kuwathibitishia Wamagharibi wanaoongozwa na Marekani kuwa haitosita kutumia silaha hizo wakati wowote usalama wake utakapokuwa hatarini. Ukweli ni kuwa, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, dunia imezidi kutumbukia kwenye jinamizi la vita vya nyuklia ikiwa ni mara ya kwanza tangu baada ya vita baridi.

Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki (NPT) ambao ulianza kutekelezwa mwaka 1970, ndio mkataba wenye wanachama wengi zaidi katika upande wa kukabiliana na uzalishaji na matumizi mabaya ya silaha. Nchi 191 zimetia saini mkataba huo. Tangu ulipoanza kutekelezwa mkataba huo hadi hivi sasa, ajenda kuu wa Umoja wa Mataifa ni kuisafisha dunia na silaha angamizi za atomiki. Lakini pamoja na hayo nchi zinazomiliki silaha za nyuklia haziheshimu ahadi zao ndani ya mkataba huo na hiyo ndiyo changamoto kubwa inayokwamisha utekelezaji wa mkataba wa NPT. Kwa upande wake Russia inasema kuwa, kuna wajibu wa kutumiwa njia zote kuhakikisha hakutokei vita vya nyuklia duniani, lakini wakati huo huo inasema kuwa, haitosita kutumia silaha hizo iwapo itashambuliwa kwa nyuklia. Rais Vladimir Putin wa Russia amesema katika barua aliyowaandikia washiriki wa mkutano wa kuangaliwa upya mkataba wa NPT kwamba vita vya nyuklia havina mshindi na vita vya namna hiyo havipaswi kuruhisiwa kutokea wakati wowote ule.

Tunapoangalia kwa kina tutaona kuwa, dunia imekumbwa na jinamizi la vita vya silaha za nyuklia kwa miaka 77 sasa. Kadiri siku zinavyopita ndivyo madola yenye silaha za nyuklia yanavyozidi kubuni na kutengeneza silaha hatari zaidi na za maangamizi makubwa zaidi za atomiki. Nchi tano duniani ndizo zinazotambuliwa rasmi kuwa zinamiliki silaha za nyuklia nazo ni Marekani, Russia, China, Ufaransa na Uingereza. Ziko nchi nyingine zimeingia kwenye kundi hilo la kumiliki silaha za atomiki katika miongo ya hivi karibuni, na kila moja inaendelea kujiimarisha kwa silaha hizo hatari mno kwa usalama wa dunia. Ni kwa kuzingatia hayo ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa, onyo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, la hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani ni la mahala pake kabisa na inabidi lichukuliwe kwa uzito mkubwa wa kuangamizwa kikamilifu silaha zote za atomiki ulimwenguni ndipo hapo dunia itakuwa salama.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *