Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, Nikolay Patrushev, ametangaza kuwa Marekani na Uingereza zinasajili na kuajiri magaidi wa kimataifa kwa ajili ya kushirikiana na jeshi la Ukraine katika vita dhidi ya Russia.
Patrushev, ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa makatibu wa Baraza la Usalama la Jumuiya ya Madola Huru (CIS) siku ya Alhamisi, alisema: Katikati ya operesheni maalumu za kijeshi (ya Russia nchini Ukraine), majasusi wa Marekani na Uingereza wanasajili makundi ya kimataifa ya kigaidi na kuyatuma Ukraine ili kuusaidia utawala wa Kiev vitani.
Hapo awali, Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu, alisema kuwa idadi kubwa ya mamluki wa kigeni bado wanashiriki katika vita hivyo na kwamba wanashirikiana na jeshi la Ukraine, na katika muda wa wiki mbili zilizopita, karibu 200 kati yao wameuawa katika maeneo ya vita.
Baada ya kuanza oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine mnamo Februari 2022, kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani, imetoa msaada wa kijeshi na silaha ambao haujawahi kushuhudiwa kwa Ukraine na kuanzisha kampeni pana ya kisiasa na kuweka vikwazo visivyo na kifani na vipana dhidi ya Moscow ili kuzuia jeshi la Russia kusonga mbele. Aidha madola hayo ya Magharibi yametuma mamluki na magaidi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwenda Ukraine.
Vyombo vya habari vya Magharibi na maafisa wa serikali ya Ukraine pia wamekiri kwamba vikosi vya kigeni na mamluki wanapigana bega kwa abega na jeshi la Ukraine dhidi ya Russia.
Gazeti la Washington Post lilichapisha ripoti ya kutoroka kwa mamluki kutoka mashariki mwa Ukraine mnamo Mei 2022. Ilidokezwa kuwa mamluki hao walitoroka kutokana na kuogopa kukabiliana na jeshi la Russia. Gazeti hilo lilikiri kuwa mamluki hao wa kigeni walikuwa raia wa Marekani na nchi zingine kadhaa na walikuwa wanashirikiana na jeshi la Ukraine
Kabla ya hapo, tovuti ya habari ya “Washington Freebeacon” ilikuwa imeripoti kuwa makundi yenye itikadi kali huko Amerika Kaskazini na Ulaya yalikuwa yanawatuma wapiganaji kuelekea Ukraine.
Zaidi ya hayo, baadhi ya watu wenye itikadi kali kutoka Chechnya wameenda Ukraine na wanashiriki katika vita dhidi ya Russia.
Pia ripoti ziliwasilishwa kuhusu jaribio la Uturuki kutuma wapiganaji wenye itikadi kali kutoka Syria kusaidia jeshi la Ukraine. Hatua hizi zinaendana na jitihada pana za nchi za Magharibi za kuizuia Russia kupata ushindi katika vita vya Ukraine. Nchi za Magharibi zimetumia rasilimali na uwezo wao wote, hata kwa kutumia makundi ya magaidi wenye itikadi kali huko Ukraine ili kukabiliana na jeshi la Russia.
Marekani na washirika wake wengine wa Ulaya na wasio wa Ulaya, kama Canada, Australia, na hata Japan, wanaviona vita vya Ukraine kuwa ni fursa ya kipekee ya kuiadhibu Russia na rais wake, Vladimir Putin. Marekani na waitifaki wake hasa katika muungano wa kijeshi wa NATO wamekuwa wakikabiliana na Russia kwa muda mrefu katika maeneo ya Ulaya, Asia Magharibi, Amerika Kusini na hata Arctic.
Aidha, kwa mtazamo wa viongozi wa nchi za Magharibi, ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine karibu na ukanda NATO na jambo litakalomaanisha kufedheheshwa kwa muungano huo wa kijeshi na kupanuka kwa ushawishi na nguvu za kikanda na kimataifa za Russia, na hsuala hilo litaathiri na kubadilisha mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya kwa madhara ya nchi za Magharibi.
Kwa hiyo Marekani na waitifaki wake wamedhamiria kuzuia ushindi wa Russia kwa gharama yoyote ile, na ni kwa msingi huo ndio maana sasa wameamua kutumia magaidi wa kimataifa kukabiliana na Russia.
Mara kwa mara Russia imekuwa ikizitaja nchi za Magharibi kuwa ni upande wa pili katika vita vya Ukraine kutokana na hatua zao za kuisaidia Kiev kwa silaha nzito.
Hapo awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, alisema kuwa nchi za Magharibi zimeanzisha vita vya pande zote dhidi ya Russia. Lavrov alisema: Wanatumia zana mbalimbali, kuanzia vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja hadi propaganda za hadaa katika vyombo vya habari vya kimataifa. Lavrov aliongeza kuwa: Kambi ya Magharibi imetangaza vita kamili dhidi yetu, dhidi ya ulimwengu wote wa Russia. Hakuna hata anayeficha ukweli huu sasa.
Kwa hakika, kambi ya Magharibi, ikiongozwa Marekani, inaamini kwamba inapaswa kutumia fursa ya vita vya Ukraine ili kuidhoofisha kikamilifu Russia, na kwa sababu hii, wanafanya kila kitu kinachowezekana, ikiwa ni pamoja na kutumia magaidi, ili kuzuia Russia kufikia malengo yake katika vita vya Ukraine.