Oparesheni ya Nablos; jibu la Wapalestina kwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Walowezi wawili wa Kizayuni wamejeruhiwa na mmoja kuangamizwa katika ufyatuaji risasi wa siku ya Alhamisi iliyopita karibu na kitongoji cha walowezi wa Kiyahudi cha Homesh huko Nablos katika ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan inayokaliwa kwa mabavu.

Faraan: Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina zimezidi kuongezeka tangu ilipoingia madarakani serikali ya mseto ya Naftali Bennett na Yair Lapid mwezi Juni uliopita. Utawala huo unaendelea kufanya jinai bila ya kujali tahadhari na maonyo inayopata kutoka kwa makundi ya muqawama ya Palestina kuhusu taathira za kuzidisha machafuko na mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina.

Mashambulizi ya mara kwa mara na mtawalia, kujeruhiwa na kuuliwa shahidi raia wa Palestina, kutolewa vibali vipya kwa vya ujenzi wa vitongoji vya walowezi, kubomolewa nyumba na kuzingirwa ardhi za Wapalestina, mateso dhidi ya mateka wa Palestina na mzingiro wa Ukanda wa Ghaza, yote hayo ni kati ya uhalifu na jinai za dhahiri ambazo utawala wa Kizayuni unaendelea kuzitenda katika kipindi cha sasa.

Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupuuza maonyo na indhari za makundi ya muqawama na mapambano ya ukombozi wa Palestina imeyafanya makundi hayo yatekeleza oparesheni mbili za kufa shahidi na ile ya juzi Alhamisi usiku dhidi ya wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni. Wakati huo huo oparesheni hizo zimebeba jumbe kadhaa muhimu.

Miongoni mwa ujumbe hizo ni kuwa, utawala ghasibu wa Israel unakabiliwa na kizazi cha wanamapambano imara wa Palestina ambacho hakijarudi nyuma na kusalimu amri hata baada ya nchi kadhaa za Kiarabu zilizoamua kuanzisha rasmi uhusiano na utawala wa Kizayuni. Oparesheni mbili hizo za kujitolea muhanga zimetekelezwa na vijana wa Kipalestina. Kuongezeka mashambulizi na hujuma hizo za Wazayuni wakiwemo wanajeshi au walowezi wa Kiyahudi kunaimarisha na kuzidisha azma na irada ya vijana wa Kipalestina ya kupigania mustakbali wao ambayo ni haki yao halali na kisheria.

Kuhusiana na suala hilo, Hazim Qassim Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: “Oparesheni ya kishujaa huko Nablos dhidi ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel na walowezi wauaji kwa mara nyingine tena inathibitisha kuwa, wananchi shujaa wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wataendeleza mapambano yao halali hadi maghasibu wote watakapofukuzwa katika ardhi zote za Palestina na kuangamizwa kikamilifu walowezi wa Kizayuni.

Tariq Izzuddin Msemaji wa Harakati ya Jihad Islami amesisitiza kuwa oparesheni ya Nablos ni dhihirisho la nguvu na upinzani wa makundi ya muqawama licha ya hatua zote za kutiwa nguvuni na kusakwa kila uchao wanamapambano wa Palestina. Pamoja na hayo, mapambano yataendelea na kuenezwa katika maeneo na nyuga zote.

Ujumbe mwingine muhimu ni kuwa, hata kama kwa upande wa kiwango cha nguvu na uwezo na hususan katika uga wa zana za kijeshi na silaha za kivita ni jambo lisilowezekana kuwalinganisha Wapalestina na utawala wa Kizayuni, lakini jinai za utawala wa Kizayuni hazitapita hivihivi bila ya jibu la Wapalestina. Ndio maana Tariq Izzuddin Msemaji wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina akasema, oparesheni ya Nablos ni jibu la kawaida kutoka kwa wana wa taifa la Palestina kwa jinai zisizo na hesabu na zisizotambua mipaka za wanajeshi maghasibu na walowezi wa Kizayuni.

Nukta ya mwisho ni kuwa, oparesheni hiyo imeutia hofu na wasiwasi utawala wa Kizayuni wa Israel. Viongozi wa utawala huo wanaelewa vyema nguvu ya muqawama na waungaji mkono wake na pia hasara na uharibifu waliopata kufuatia oparesheni hizo za kujitolea mhanga na kufa shahidi. Kwa msingi huo, Beny Gantz Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametangaza katika radiamali yake kwa oparesheni ya Nablos kuwa wataendelea kujiweka tayari dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan. Televisheni ya al Mayadeen pia imeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umeongezeka idadi ya wanajeshi wake katika maeneo ya kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *