Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeanzisha tena msukumo wake wa kutaka uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa (UN) huku Marekani ikiendeleza njama zake za muda mrefu za kupinga hatua hiyo.
“Tunajadiliana kwa nia njema na wanachama wote Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” amesema Riyad Mansour, balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa huku akiwa na matumaini kuwa mara hii watafanikiwa.
Mansour katika wiki kadhaa zilizopita ameanzisha mashauriano na wajumbe wa Baraza la Usalama juu ya uwezekano wa Palestina kupata uanachama kamili, hatua ambayo imeonekana kama jaribio la kuvunja mkwamo katika mchakato wa amani.
Marekani, ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa utawala ghasibu wa Israel, unaokoloni ardhi za Palestina, ikiwa ni miongoni mwa wanachama watano wa kudumu wa UNSC wenye kura ya turufu, siku za nyuma ilipinga Palestina kuwa mwanachama kamili.
Mansour alisema kutokana na kwamba mchakato wa amani umesitishwa kwa miaka minane na kwamba hakuna mpango wowote mezani, suala la uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa linapaswa kusonga mbele.
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti hapo awali kwamba utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden uliihimiza Mamlaka ya Palestina kutofikisha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ombi la kupata uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kuwa kuna uwezekano wa kupinga hatua hiyo.
Mnamo mwaka wa 2012, Umoja wa Mataifa ulipandisha hadhi ya Palestina hadi ile ya “nchi isiyo mwanachama”, hatua ambayo iliinua hadhi ya Palestina katika umoja huo.
Katika wiki za hivi karibuni, Israel imeongeza mashambulizi katika vijiji na miji ya Palestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Kutokana na mashambulizi hayo makumi ya Wapalestina wamepoteza maisha na wengine wengi kukamatwa.
Israel iliikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds (Jerusalem) Mashariki wakati wa Vita vya Siku Sita mwaka 1967. Baadaye ilitwaa eneo la Quds Mashariki katika hatua isiyotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
Wapalestina wanataka utatuzi wa mzozo na Tel Aviv kulingana na kile kinachoitwa suluhisho la serikali mbili pamoja na mipaka ya kabla ya 1967. Hata hivyo viongozi madhalimu wa Israel wanasisitiza kudumisha ukaliaji kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Duru ya mwisho ya mazungumzo kati ya Israel na Palestina ilisambaratika mwaka 2014. Miongoni mwa mambo muhimu yaliyofelisha mazungumzo hayo ni kuendelea kwa Israel katika shughuli za ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.