Paris yamwita nyumbani balozi wake baada ya wanajeshi wake kutimuliwa Burkina Faso

Baada ya serikali ya Burkina Faso kuiamuru Ufaransa iondoe wanajeshi wake katika kipindi cha mwezi mmoja ujao, mkoloni huyo kizee wa Ulaya amehamakishwa na hatua hiyo na ameamua kumrudisha nyumbani balozi wake kutoka Ouagadougou.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Fars, siku moja baada ya Ufaransa kusema kuwa itaheshimu uamuzi wa serikali ya Burkina Faso na itaondoa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Paris ilitangaza ja Alkhamisi Januari 26, 2023 kwamba imeamua pia kumwita nyumbani balozi wake aliyeko Burkina Faso.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetangaza: Tumeamua kumrudisha Paris balozi wetu kutoka Burkina Faso kutokana na matukio yaliyojiri hivi karibuni. Tumemwita nyumbani ili kushauriana naye zaidi.

Jumatatu wiki hii, Burkina Faso ilitangaza kuwa imeipa Ufaransa muda wa mwezi mmoja kuondoa vikosi vyake vyenye karibu wanajeshi 400 nchini humo, na juzi Jumatano Paris ilisema itatekeleza amri hiyo. Jana Alkhamisi, Paris ilitangaza kumwita nyumbani balozi wake kutoka Ouagadougou ikiwa ni ishara ya wazi ya kutofurahishwa mkoloni huyo kizee wa Ulaya na uamuzi huo wa Burkina Faso.

Uamuzi wa Burkina Faso  wa kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa ni ushahidi wa kuzidi kuzorota uhusiano kati ya Ufaransa na koloni lake la zamani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2022. Baadhi ya mivutano hiyo inatokana na ukweli kwamba uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Burkina Faso haujaimarisha usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na wananchi wa Burkina Faso wanaamini kwamba ni wakoloni hao wa Ulaya ndio wanaochochea machafuko, mapinduzi ya mfululizo ya kijeshi, vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *