Polisi Kenya yamkamata tena mshukiwa wa mauaji huko Marekani

Polisi ya Kenya imetangaza kuwa imemkamata tena Kevin Kinyanjui Kang’ethe aliyetoroka katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga alimokuwa akizuiliwa baada ya ubalozi wa Marekani kuomba Kenya isaidie kumsafirisha hadi nchini humo ili akashtakiwe kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake na kisha kuutupa mwili wake kwenye uwanja wa ndege.

Kutoroka gerezani Kinyanjui Kang’ethe akiwa mikononi mwa polisi kulizua mjadala mkubwa kwenye taifa hilo baada ya awali kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.

Kevin Kang’ethe alizuiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Muthaiga jijini Nairobi akisubiri kurejeshwa nchini Marekani kutokana na kifo cha Margaret Mbitu, ambaye mwili wake ulipatikana katika maegesho ya magari ya uwanja wa ndege mwaka jana, lakini akatoroka kutoka kituo cha polisi wiki iliyopita kwa njia isiyoeleweka.

Kamanda wa polisi jijini Nairobi, Adamson Bungei, amesema Kang’ethe alikuwa amejificha katika nyumba ya jamaa yake viungani mwa jiji la Nairobi, ambapo polisi walimpata jana Jumanne jioni baada ya msako wa siku kadhaa.

Kwa sasa mshukiwa huto amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutoroka kizuizini wakati akisubiri kurejeshwa nchini Marekani.

Mamlaka za Marekani na Kenya zilikuwa zimeanzisha msako baada ya Mbitu kupatikana akiwa ameuawa kwa kuchomwa kisu kwenye maegesho ya magari katika uwanja wa ndege wa Boston wa Logan mwezi Novemba.

Hati ya kukamatwa kwa Kang’ethe ilitolewa baada ya kutoroka Marekani kuelekea Kenya, ambako alikamatwa mwishoni mwa Januari.

Maafisa wanne wa polisi, jamaa wawili na wakili wa mshukiwa walikamatwa kuhusiana na kutoroka kwake gerezani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *