Shirika huru na lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu limesema kuwa, wanajeshi wa Israel wamewatia mbaroni Wapalestina 6,500 wakiwemo mamia ya wanawake na watoto katika eneo lote la Ukingo wa Magharibi linaokaliwa kwa mabavu tangu mwanzoni mwa mwaka huu, huku utawala wa Israel ukiendelea na kampeni yake ya kuwanyanyasa na kuwatia mbaroni Wapalestina.
Klabu ya Wafungwa wa Kipalestina (PPC) imesema katika taarifa yake kuwa wanawake 153 na watoto 811 ni miongoni mwa waliozuiliwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa amri 2,134 za kuzuiliwa kiutawala pia zilitolewa dhidi ya wafungwa wa Kipalestina katika kipindi hicho.
Wale wanaoitwa wafungwa wa kiutawala wanakamatwa kwa “ushahidi wa siri”, bila kujua mashtaka dhidi yao, na hawaruhusiwi kujitetea mahakamani. Kwa kawaida hushikiliwa kwa muda wa miezi sita inayoweza kurefushwa, na mara nyingi hupelekea kufungwa kwa miaka kadhaa.
PPC imesema kwamba Wapalestina 4,700 kwa sasa wanazuiliwa katika magereza 23 na mahabusu zinazosimamiwa na Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limebainisha kuwa wafungwa hao wa Kipalestina wanajumuisha mahabusi 34 wa kike, watoto 150 pamoja na wafungwa 835 wa kiutawala.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba wafungwa 600 wa Kipalestina pia wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya muda mrefu, ikisisitiza kuwa wanakabiliana na hali mbaya, kutendewa unyama na mateso makali.
PPC ilisema wafungwa wote wa Kipalestina wanazuiliwa katika mazingira ya kinyama, hawapati huduma muhimu za kimatibabu, na wanatelekezwa kwa makusudi.