DAR ES SALAAM: Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 katika fasihi, Prof. Abdulrazak Gurnah, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.
Hafla hiyo itafanyika kesho katika ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Aprili 12, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inayoratibu utoaji wa tuzo hiyo, Dk Aneth Komba, amesema kuwa Profesa Gurnah atawasili nchini leo kwa mwaliko rasmi wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda.
Amesema moja ya malengo ya tuzo hiyo ni kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kazi kubwa aliyoifanya kwenye eneo la uandishi.
Dk Komba amesema kabla ya hafla ya tuzo hiyo, Prof.Gurnah atapata nafasi ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na waandishi bunifu nchini kwa lengo la kubadilishana nao mawazo kuhusu uandishi bunifu.
Amesema mbali na Gurnah wageni wengine katika hafla hiyo ni waandishi maarufu kutoka nchi za Kenya na Uganda, ambao wataungana na waandishi bunifu wa Tanzania katika hafla ya tuzo hiyo na watapata nafasi ya kutoa uzoeafu wao katika eneo la uandishi bunifu .
Prof. Gurnah ni mwandishi wa fasihi na alikuwa mshindi katika tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 iliyofanyika nchini Sweden.
Tuzo hiyo ya Taifa inajumuisha vipengele vya Riwaya, Ushairi na Hadithi za Watoto ambapo washindi wa kwanza katika vipingele hivyo watapata zawadi ya Sh milioni 10.
Tuzo hiyo inafanyika nchini kwa mara ya pili ambapo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 2023 na mshindi alikua Mhariri wa HabariLEO, Hamis Kibari