Rais wa Russia ametangaza kuwa Moscow haitaziruhusu nchi za Magharibi kuwatumia watu wa Ukraine kwa ajili ya kuigawa na kuidhoofisha Russia.
Katika hotuba yake ya kufunga mwaka wa 2022, Rais wa Russia, Vladimir Putin ameutaja mwaka uliomalizika wa 2022 kuwa ulikuwa mwaka uliojaa matukio ambayo ni msingi wa mustakabali wa uhuru na kujitawala kikamilifu nchi yake.
Kuhusu mgogoro wa Ukraine na operesheni za kijeshi za nchi hiyo, Rais wa Russia amesema kuwa, kwa miaka mingi nchi za Magharibi ziliiarifu Russia kuwa zina malengo ya amani; lakini uukweli ni kuwa zinawaunga mkono Wanazi mamboleo.
Putin amesema kuwa nchi za Magharibi zinawatumia watu wa Ukraine kuigawa na kuidhoofisha Russia, na kwamba nchi hiyo kamwe haitaruhusu jambo hilo.
Wakati huo huo Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Russia anaamini kuwa nchi za Magharibi zimejaribu kuidhoofisha Russia tangu baada ya kumalizika kwa Vita Baridi.
Leonid Slutsky amesema kuwa, makubaliano ya Minsk yalikuwa sehemu ya mkakati huo.
Russia ilianzisha operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine mapema mwaka huu. Moscow imetangaza kwamba, itasitisha operesheni hiyo ya kijeshi iwapo itapewa dhamana na kuhakikishwa kwamba Kiev si tishio la kijeshi. Vilevile inataka kuondoka madarakani Wanazi Mamboleo katika nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.