Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema nchi yake iko tayari kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sheikh Muhammad bin Abdurahman Al Thani ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo aliyofanya na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian pembeni ya mkutano wa 58 wa usalama wa Munich ulioanza jana nchini Ujerumani.
Sheikh Abdurahman Al Thani, ambaye pia na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar amesema, Doha inasubiri kwa hamu ugeni wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akaelezea ratiba zilizoandaliwa kwa ajili ya ujumbe wa Tehran na utayari wa nchi yake kuitumia safari hiyo kwa ajili ya kustawisha zaidi uhusiano baina ya nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo, waziri wa mambo ya nje wa Qatar, mbali na kukaribisha hatua iliyopigwa katika mazungumzo ya Vienna na kuyaelezea matokeo ya mazungumzo hayo kuwa yenye umuhimu mkubwa kwa eneo, amebainisha pia kuhusu hatua ilizochukua Qatar kuhusiana na kadhia ya Afghanistan na mazungumzo yanayoendelea hivi sasa baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ametilia mkazo umuhimu wa uhusiano wa kupigiwa mfano wa nchi mbili na akasema, ana matumaini kuwa safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Qatar ya kushiriki pia katika kikao cha OPEC ya Gesi itakuwa ya mafanikio katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Seyyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kuelekea Doha siku ya Jumatatu kwa mwaliko rasmi uliotolewa na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani…/