Radiamali hasi ya Madola ya Magharibi ya kunyongwa jasusi wa Uingereza nchini Iran

Kunyongwa Ali Reza Akbari, jasusi wa shirika la kijasusi la Uingereza la MI6 kumekabiliwa na matamshi ya pupa na radiamali tofauti na hasi za madola ya Magharibi. Radiamali hizo zinaonyesha kupata pigo kubwa mipango ya kijasusi ya Magharibi dhidi ya Iran.

Jumamosi ya jana tarehe 14 Januari, Idara ya Mahakama ya Iran, ilitangaza kuwa, Akbari aliyekuwa na uraia pacha wa Iran na Uingereza amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ufisadi mkubwa katika ardhi na kuendesha vitendo vya kuhatarisha usalama wa ndani na nje ya Iran kupitia kulifanyia ujasusi shirika la kijasusi la Uingereza MI6.

Kutangazwa habari ya kutekelezwa hukumu ya kunyongwa jasusi huyo sio tu kwamba, kumefuatiwa na radiamali ya uingiliiaji masuala ya ndani ya viongozi wa Uingereza na Ulaya, bali Robert Malley, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran ambaye baada ya kuibuka machafuko ya ndani hapa nchini  alijikita zaidi katika suala hilo, naye ametoa matamshi yake na ya serikali ya Biden ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameshindwa kuzuia na kuficha hamaki zake baada ya jasusi wa nchi hiyo kutiwa mbaroni na kunyongwa nchini Iran na amedai kuwa, kunyongwa jasusi huyo ni kitendo cha kikatili na cha woga.

Katika ujumbe wake wa twitter, Waziri Mkuu wa Uingereza hakuashiria hata kwa mbali ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na madola ya Magharibi na badala yake ametoa matamshi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran kwa kudai kwamba, kunyongwa jasusi huyo nchini Iran ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu.

James Cleverly, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza alitangaza jana kuwa, serikali ya London imemuita nyumbani balozi wake mjini Tehran eti kwa ajili ya mashauriano, kufuatia hatua ya Idara ya Mahakama ya Iran kumnyonga Ali Reza Akbari, aliyekuwa jasusi wa shirika la kijasusi la Uingereza la MI6.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amedai kuwa, ‘Jibu letu kwa Iran haliishii kwa hatua ya leo (ya kumrejesha nyumbani balozi wake wa Tehran kwa muda usiojulikana). Tunatathmini hatua zaidi ya kuchukua (dhidi ya Iran).”

Aidha Uingereza imetangaza kumuwekea vikwazo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran, Mohammad Jafar Montazeri kutokana na kuhamakishwa na hatua ya Iran kumnyonga jasusi huyo wa MI6 ya Uingereza.

Jana pia Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimwita balozi wa Uingereza mjini Tehran, Simon Shercliff, kutokana na uingiliaji wa London katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwanadiplomasia huyo wa Uingereza aliitwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika Wizara hiyo, ambapo Tehran ilimbainishia kuwa inalaani vikali uingiliaji wa Uingereza katika masuala ya ndani ya Iran, hususan masuala yanayofungamana na usalama wa taifa.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akiwa pamoja na mshirika wake Uingereza katika kulifanya kuwa la kisiasa faili la kimahakama, ameonyesha radiamali yake ya kunyongwa jasusi Ali Reza Akbari. Katika matamshi yake ya kuingilia masuala ya ndani ya taifa jingine, Macron amesema: Tutalaani kunyongwa jasusi wa Uingereza nchini Iran. Macron ameonyesha kuwa pamoja na Uingereza katika kadhia hii.

Radiamali hazi za madola ya Magharibi na kulaani hatua ya Iran ya kumnyonga jasusi wa Uingereza sio kitu ambacho hakikutarajiwa. Tukitupia jicho orodha ya makosa na uhalifu wa usalama wa taifa na hatua za kijasusi za Ali Reza Akbari tutaona ni kwa namna gani hatua zake za kihalifu na kijinai zilikuwa na thamani kubwa kwa Uingereza na ndio maana viongozi wake wamehamaki na wanabwabwaja ovyo.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, kwa miaka kadhaa, Akbari alichukua hatua zilizo dhidi ya usalama wa taifa wa Iran na alifanya ujasusi kwa maslahi ya serikali ya Uingereza. Alikuwa na uhusiano na Shirika la Kijasusi la M16 la Uingereza na alifanya mikutano kadhaa na maafisa wa kijasusi wa adui katika nchi mbalimbali. Ali Reza Akbari, kwa muda mrefu aliendeleza ujasusi ambao ni uhaini dhidi ya usalama wa ndani na nje ya Iran ambapo shughuli zake hizo za ujasusi zilivuruga pakubwa nidhamu ya umma nchini Iran.

Vyovyote itakavyokuwa, suala muhimu ni kuwa, hatua madhubuti zilizochukuliwa na Iran zikiwemo za vyombo vya kiintelijesia na Idara ya Mahakama katika kushughulikia kadhia ya Ali Akbar ni ishara ya wazi ya azma thabiti ya taifa hili katika uga wa kukabiliana na harakati na hatua za kijasusi za kigeni na wakati huo huo kuwa macho na kufuatilia hatua kwa hatua nyendo za watu wenye kutiliwa shaka na hususan kuhusiana na vyombo vya kijasusi vya kigeni. Hapana shaka kuwa, kunyongwa Ali Reza Akbari ni sawa na indhari na onyo kali kwa vyombo vya kijasusi vya kigeni kuhusiana na njama zao za kutaka kupenya na kuingia Iran kwa ajili ya kuchota taarifa muhimu za taifa hili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *