Mamia ya waandamanaji walikusanyika jana Jumamosi nje ya uwanja wa michezo wa Samuel Kanyon Doe mjini Monrovia kupinga kupanda kwa gharama za maisha, siku moja kabla ya Rais George Weah kurejea leo nchini baada ya kukamilisha safari ya siku 48 nje ya nchi.
Maandamano hayo yaliandaliwa na muungano wa vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Waandamanaji hao walikusanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji la Monrovia wakitoa nara za kupinga serikali huku wakiwa na mabango yenye maandishi “Tumechoka na Tunateseka”.
Tangu mapema mwezi huu wa Disemba, bei ya mchele, chakula kikuu cha Libeŕia, iliongezeka kutoka dola 15 hadi dola 17.50 kwa kila gunia la kilo 25. Ongezeko hili la bei ya mchele limetokana na uhaba wa bidhaa hiyo ambao umesababisha foleni ndefu na kupanda kwa bei ya vyakula mbalimbali, kwa sababu ya usumbufu wa usambazaji wa kimataifa unaochangiwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Kulingana na Shiŕika la Mpango wa Chakula Duniani, wastani wa asilimia 64 ya watu nchini Libeŕia – moja ya nchi maskini zaidi duniani – wanaishi chini ya mstari wa umaskini, na milioni 1.3 kati yao wanaishi katika umaskini uliokithiri.
Maandamano ya wapinzani nchini Liberia yamefanyika siku moja kabla ya Rais wa nchi hiyo, George Weah, kurejea nchini leo Jumapili akitokea nchi za nje ikiwemo Qatar, alikokwenda kutazama mwanawe akiichezea timu ya taifa ya soka ya Marekani katika Kombe la Dunia la FIFA 2022.
Weah, nyota wa zamani wa kandanda wa Afrika, ambaye ndiye Mwafrika pekee aliyeshinda tuuzo ya Ballon d’Or mwaka wa 1995 ya mchezaji bora wa dunia, alizitembelea pia Morocco, Misri na Ufaransa.