Rais wa muda mrefu wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliapishwa Alhamisi kwa muhula wa sita.
Obiang, mwenye umri wa miaka 80, alizungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwake na kusema, “Maadamu mimi ni rais, na kwa msaada wa rasilimali zetu, matakwa ya watu na mahitaji yao ya ustawi yatatimizwa kikamilifu.”
Kuapishwa kwake kulifanyika katika mji mkuu, Malabo, na kuashiria mwanzo wa muhula wake mpya wa miaka saba katika uongozi wa nchi.
Sherehe hiyo ilianza baada ya gwaride la kijeshi lililohudhuriwa na maafisa wa kitaifa na viongozi wengi wa mataifa ya kigeni barani Afrika.
Obiang ameahidi utekelezaji kamili wa miradi bora, pamoja na kutokomeza ufisadi na kudumisha umoja wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Amesisitiza amani na utulivu wake, pamoja na maendeleo endelevu ambayo amesema taifa linaendelea kupata.
“Takwimu zinaonyesha kuwa watu daima wameunga mkono kugombea kwangu,” amesema Obiang, rais aliyekaa muda mrefu zaidi madarakani duniani ambapo huu ni mwaka wa 43 wa uongozi wake.
Obiang amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1979, wakati alipong’olewa madarakani mtangulizi wake Francisco Macias Nguema kupitia mapinduzi.
Uchaguzi wa hivi punde zaidi wa rais nchini humo ulifanyika Novemba 20 na matokeo rasmi yalionyesha kuwa Obiang alipata ushindi mkubwa wa karibu asilimia 95 katika nchi hiyo yenye wakazi wapatao milioni 2.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Uchaguzi, Chama chake cha Kidemokrasia cha Guinea ya Ikweta (PDGE) kilishinda viti vyote 588 katika mabaraza ya manispaa, viti vyote 55 katika Seneti na viti vyote 100 katika Baraza la Wawakilishi.
Licha ya kuwa muuzaji mafuta wa tatu kwa ukubwa katika Afŕika iliyo Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, idadi kubwa ya wakazi wa Equatorial Guinea kwa sasa wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kulingana na Benki ya Dunia.