Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kwamba mtandao wa kijamii wa Facebook utafunguliwa tena nchini humo ikiwa utaacha kile alichokitaja kuwa ni “kucheza michezo.”
Facebook ilipigwa marufuku nchini Uganda kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021 baada ya kutuhumiwa kuchochea ghasia nchini humo.
Akizungumza Ijumaa na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari vya Uganda, Rais Museveni amesema: “Facebook wana kiburi. Walikuwa wakitumiwa kutushambulia. Watu wetu walipojaribu kujibu walifunga akaunti zetu. Natumai Facebook sasa inafahamu nani anaiongoza Uganda! Watakapoacha kucheza michezo tutawaruhusu.”
Rais Museveni aidha amesema baada ya Facebook kutimuliwa Uganda, maisha ya wananchi yanaendelea kama kawaida bila tatizo lolote kwa hivyo mtandao huo wa kijamii hauathiri maisha ya wananchi.
Matamshi ya Rais Museveni yanakuja siku chache baada ya kaimu mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), Bi Irene Kagwa kusema serikali inasubiri Facebook, ambayo sasa inaendeshwa na shirika la Meta, kutatua masuala ambayo hayajakamilika kabla ya kufunguliwa tena kikamilifu.
Ameongeza kuwa, “Kwa upande wetu, tunangojea Facebook. Tulizungumza na tukahitimisha. Kwa hiyo, masuala yaliyosalia yapo upande wao. Kama serikali, tuko tayari kuirejesha mara tu watakapotimiza ahadi zao.”
Kabla ya kusimamishwa Januari 2021, serikali ya Uganda ilikuwa imehitilafiana na mtandao wa Facebook, ikishutumu kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii kwa kutochukua hatua za kudhibiti matamshi ya chuki, uwongo na kuvuruga umoja wa taifa la Uganda.