Rais Mwinyi aeleza njia EAC kufurahia Kiswahili duniani

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema namna bora ya kuonyesha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imefurahi kuwa na siku ya lugha ya Kiswahili duniani ni kuongeza jitihada za kuimarisha lugha hiyo kwa kubuni mbinu bora za kukuza na kuiendeleza.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamis Julai 7, 2022 katika maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili duniani ambapo kwa mara kwanza yameadhimishwa baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kutangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Rais Mwinyi amesema wajibu wa kwanza kuonyesha mapenzi ya lugha hiyo ni kuizungumza kwa ufasaha na usahihi ili kuwa walimu wazuri wa wale wanaojifunza.

“Kadhalika taasisi zinazosimamia maendeleo ya Kiswahili nazo zina wajibu wa kushirikiana katika masuala ya kendeleza lugha hiyo kwa kutoa mafunzo na kufanya tafiti za isimu na fasihi na kuwasaidia watunzi wa vitabu na machapisho yatakayotumiwa kukuza Kiswahili,” amesema

Amesema kutokana na kukua kwa lugha hiyo kumeongeza mahitaji ya wataalamu wa lugha hiyo duniani wakiwemo walimu, waandishi wa vitabu, wakalimani na watangazaji wa vyombo vya habari vinavyotangaza kwa lugha ya kswahili.

Hali hiyo inakaribisha fursa pana za ajira kwa wataalamu wa lugha hiyo hivyo lazima kuwe na mikakati madhubuti katika nchi zao na vyuoni katika kuandaa wahitimu bora wa kwenda kuzishika nafasi hizo.

Wakitoa salaam kutoka kwa mabaraza ya Kiswahili; Bakiza na Bakita, Mwanahija Juma na Dk Rizat Mmari Hassan wamesema maadhimisho hayo yana umuhimu kwa mataifa hayo katika jitihada za kukuza na kuendeleza Kiswahili.

Dk Rizat kutoka Bakita amewashauri nchi wanachama kuanzisha mabaraza kama hayo ya Kiswahili ili kuwa na mikakati mizuri kuendeleza Kiswahili na ikiwa watapata changamoto watawasaidia katika kuyaunda mabaraza hayo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, amesema kuadhimisha siku hiyo kwa mara ya kwanza Zanzibar ni historia ya pekee katika kukuza utamaduni wa Mwafrika kwani lugha hiyo ni ya kwanza kwa Afrika na ya nane duniani kwa kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Steven Mlote, amesema wanapaswa kuongeza kasi kukitangaza na kukitumia Kiswahili katika shughuli zote za Afrika Mashariki.

Wawakilishi wa Nchi wanachama kutoka nchi za Burundi, Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini, kwa nyakati tofauti walisema serikali zao zimekuwa na maendeleo makubwa katika kuendeleza kiswahili kisera na kimatumizi katika nchi zao na hata kufundishwa katika shule na vyuo vikuu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *