Rais Vladmir Putin wa Russia ameshutumu vikwazo vilivyowekwa na madola ya magharibi dhidi ya Russia akisema ni hatari kwa dunia nzima.
Putin ameyasema hayo wakati wa hotuba yake kwenye Kongamano la Uchumi la Mashariki katika mji wa bandari wa Mashariki ya Mbali wa Vladivostok leo Jumatano, na kuongeza kuwa madola ya Magharibi yamehujumu uchumi wa dunia kwa jaribio la “kichokozi” la kulazimisha utawala wake duniani kote.
Amesema vikwazo vya madola ya Magharibi ni majaribio ya wazi ya Magharibi ya kulazimisha sera zao kwa nchi zingine, sambamba na kuziondolea uhuru wao.
Putin amesema nchi za Magharibi zimekuwa zikisita kutambua mabadiliko makubwa yasiyoweza kutenguliwa katika uhusiano wa kimataifa. Amesema licha ya mabadiliko hayo nchi za Magharibi zinajaribu kudumisha utaratibu wa zamani wa ulimwengu ambao uliwanufaisha wao tu.
Rais wa Russia ameendelea kusema nchi yake imebaini kuwepo fursa zaidi katika kuingia katika masoko ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kufuatia kuwekewa vikwazo vikubwa vya nchi za Magharibi kutokana na oparesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.
Putin amesisitiza kuwa hakuna atakayeweza kuitenga Russia na kuongeza kuwa operesheni za kijeshi nchini Ukraine zimelenga kuimarisha mamlaka ya Russia.
Pia amesema Russia imefanya kila iwezalo kuhakikisha Ukraine ina uwezo wa kuuza nafaka nje ya nchi huku vita vikiendelea.
Rais wa Russia ameonya kwamba matatizo katika soko la chakula duniani huenda yakaongezeka, akiongeza kuwa janga la kibinadamu linakaribia.
Tangu kuanza kwa “operesheni maalumu ya kijeshi” ya Russia nchini Ukraine mnamo Februari 24, Marekani na washirika wake wa Ulaya wameiwekea vikwazo ambavyo vimepelekea kuongezeka bei ya nishati na nafaka duniani.
Aidha hatua ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ya kushadidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Russia na kupeleka shehena za silaha nyepesi na nzito nchini Ukraine, si tu haijasaidia kutuliza hali ya mambo, bali imekoleza zaidi moto wa vita ndani ya nchi hiyo ya Ulaya