Rais Ruto afanya mabadiliko serikalini Kenya, awateua wandani wa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta

Rais William Ruto wa Kenya amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kwa kuwateua watu wa karibu kwa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta kushika nyadhifa kwenye serikali yake.

Duru za habari za Kenya zimeandika kuwa, washirika wa karibu wa Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta, Mutahi Kagwe na Lee Kinyanjui na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, wameteuliwa mawaziri katika mabadiliko yaliyofanywa jana Alkhamisi na Rais William Ruto.

Rais Ruto alisema kwamba, mabadiliko hayo ambayo yanafanyika wiki moja baada ya handisheki yake na Bw Kenyatta, wakati alipomtembelea nyumbani kwake Ichaweri, yananuiwa kuimarisha utoaji wa huduma.

Amesema, mabadiliko hayo yanalenga kurekebisha Wizara ili kuboresha utendakazi na kuimarisha utoaji wa huduma kama ilivyoainishwa katika mpango wa Utawala wa Kenya Kwanza chini ya Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya kuanzia mashinani.

Kwa kuteua washirika wa Bw Kenyatta katika Serikali yake, Rais Ruto anaonekana kutaka kurejesha ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya ulioyeyuka baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu rais, Rigathi Gachagua.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *