Rais William Ruto wa Jamhuri ya Kenya leo aliwaongoza Wakenya kusherehekea Siku ya Mashujaa yaliyotilia mkazo mpango wa afya bora kwa wote, huku watu wanne wakiripotiwa kuaga dunia kutokana na mkanyagano kwenye maadhimisho hayo.
Akihutubia katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa mjini Kericho, Rais Ruto Rais alizindua mpango mpya wa huduma ya afya kwa wote uitwao “Afya Nyumbani”.
Uzinduzi huu unafuatia hatua ya Rais Ruto ya kuidhinisha sheria nne mpya, ambazo zingetumika kuendesha shughuli za afya kote nchini huku akisisitiza kuwa, serikkali yake “imetenga kiasi cha shilingi bilioni tatu kila mwaka kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la mpango huo.
Serikali ya Kenya inasema inatilia mkazo kuzuia magonjwa na vile vile kuwapa nafasi Wakenya wote kuchangia mfumo mpya wa afya.
Hata hivyo, viongozi waliohudhuria kwenye sherehe hiyo hawakusita kuibua masuala ya kisiasa, ikizingatiwa kuwa sherehe yenyewe ilifanyika katika ngome ya Rais Ruto.
Naibu Rais Rigathi Gachagua alitumia fursa ya hotuba yake kuonesha nguvu za serikali yao, akiwakosoa wapinzani kwamba, hawana mawazo ya maendeleo.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Mashujaa yalivutia umati mkubwa wa watu ambapo baadhi yao walikesha nje ya uwanja wa usiku wa kumkia leo ilimradi wasikose nafasi.
Hata madhimisho hayo yaliingia dosari baada ya watu wanne kupoteza maisha katika mkanyagano. Msongamano wa asubuhi ulisababisha mkanyagano na polisi wamethibitisha kuwa, watu wanne wamefariki dunia na zaidi ya kumi kujeruhiwa kwenye mkanyagano huo. Majeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Kericho kwa ajili ya matibabu.