Rais Ruto aliyasema hayo jana Jumanne, akiwa katika Kaunti ya Nyandarua huku akiwajia juu maafisa wa mahakama ambao amesema kazi yao ni kusimamisha miradi kupitia ilani za mahakama.
“Ninaheshimu uhuru wa mahakama, lakini kile sitakubali na naapa kukisimamisha ni utundu, ukiritimba na ufisadi wa wachache ndani ya idara hiyo kwa kuwa walio na uwezo kwa mujibu wa katiba ni wananchi wenyewe,” akasema Rais Ruto.
Vilevile amewaagiza mawaziri na makatibu wizara wajiandae kuanza kutekeleza miradi ambayo imepitishwa na wananchi na mabunge yao na kuwa sheria.
“Mpango wa ujenzi wa nyumba, ule wa afya kwa wote…barabara ambazo zinanuia kusaidia Wakenya…enda weka pesa tuanze utekelezaji,” amesema.
Rais wa Kenya amesema kuwa ajenda yake imetekwa nyara na “mitandao ya ufisadi iliyoenea hadi mahakamani ambako kuna wachache washirika wa kuhongwa ili wakwamishe yale ya kuwafaa Wakenya kwa masilahi ya wachache”.
Matamshi hayo ya Rais William Ruto wa Kenya yamekemewa vikali na aliyekuwa rais wa Muungano wa Mawakili nchini Kenya (LSK) Bw Okong’o Omogeni huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa ushuru wa ujenzi nyumba tarehe 14 mwezi huu wa Januari.
Okong’o Omogeni ameitaka Idara ya Mahakama isitishike na matamshi hayo na kumkumbusha Rais Ruto kwamba yuko chini ya taasisi kadha ikiwemo mahakama na kwamba kujaribu kukaidi mfumo wa kisheria ni kukaribisha mtafaruku mkubwa nchini.