Rais Samia amteua Jenerali Mabeyo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Zuhura Yunus imesema kuwa uteuzi huo umeanzia leo Alhamisi Juni 30, 2022.

Uteuzi huo umekuja muda mfupi baada ya Mkuu huyo wa nchi kumuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) mpya, Jenerali Jacob Mkunda.

Wakati wa uapisho huo uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alimshukuru huku akiahidi kumpangia majukumu mengine Mabeyo.

“Namshukuru Mungu kwa kumjalia Jenerali Mabeyo kumaliza kazi leo akiwa smart na bado ana nguvu. Nikushukuru Jenerali Mabeyo kwa kazi nzuri uliyofanya katika utumishi wako wa zaidi ya miaka 40 jeshini.

“Umefanya kazi yako kwa uadilifu mkubwa, umetumikia cheo chako kwa jitihada kubwa na umemaliza na kukabidhi kwa wengine. Tunakushukuru sana na tunakupongeza sana kwa sababu siyo kazi rahisi,” amesema Rais Samia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *