Rais Gustavo Petro wa Colombia ameiasa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa waranti wa kumtia nguvuni Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.
Rais wa Colombia alitoa mwito huo jana Ijumaa katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: Benjamin Netanyahu hawezi kusimamisha mauaji ya kimbari, na kwa msingi huo, kuna haja ya kutoa waranti dhidi yake.
Kadhalika Gustavo Petro amelitaza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litume kikosi cha kulinda amani katika Ukanda wa Gaza.
Ikumbukwe kuwa, Mei Mosi, Rais wa Colombia alisema alipohutubia maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani katika mji mkuu wa nchi hiyo Bogota kuwa, nchi yake imeamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Gustavo Petro alisisitiza kuwa, serikali ya Bogota imechukua uamuzi huo kwa sababu ya utawala wa Kizayuni kuwa na rais muhusika wa mauaji ya kimbari.
Mashinikizo ya kuitaka ICC imkamate Netanyahu yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Marekani wameanzisha kampeni kubwa ya kuzuia hatua yoyote ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa kibali cha kukamatwa viongozi watenda jinai na mauaji ya kimbari wa Israel, hususan Netanyahu.