Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuhusu misimamo ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu lilivyowekewa taifa hili.
Seyyid Ebrahim Raisi ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.
Katika mazungumzo hayo, Rais Raisi ameashiria ripoti kadhaa na rasmi za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zilizoonyesha kwamba mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima umekuwa ukiendeshwa kwa uwazi na katu haujakengeuka mkondo wa sheria na akabainisha kuwa, kuibua kila mara tuhuma na madai yayo kwa yayo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa mazungumzo, kunadhihirisha jinsi mchakato wa mazungumzo unavyotumiwa kwa malengo ya kisiasa.
Seyyid Ebrahim Rais amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavitambua vikwazo vya upande mmoja ilivyowekewa kuwa ni vya kidhalimu, si vya kisheria wala si vya haki na akasisitiza kuwa, Tehran imeazimia kwa dhati kutetea haki zake na kwamba jitihada zote inapasa zielekezwe katika kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa na kunakuwepo hakikisho linalohitajika juu ya suala hilo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha pia kwamba ili kupatikana mwafaka thabiti na endelevu ni lazima vikwazo viondolewe na madai yasiyo na msingi wala mashiko yatupiliwe mbali, tena bila masharti yoyote.
Kwa upande wake, Amir wa Qatar Sheiokh Tamim bin Hamad Al Thani amesema katika mazungumzo hayo aliyofanya kwa njia ya simu na Rais wa Iran kwamba nchi yake inaunga mkono misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu katika kupigania haki zake na kuendelezwa mazungumzo hasa juu ya suala la kuimarisha mashirikiano ya pande mbili za Doha na Tehran.