Rais Michel Aoun wa Lebanon amesisitiza kuwa anaiunga mkono Hizbullah na akabainisha kwamba, hatua iliyochukuliwa na muqawama wa Lebanon imesukuma mbele mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana ya kuainisha mipaka ya bahari.
Mzozo kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Lebanon kuhusu mipaka ya bahari ya pande hizo mbili umeongezeka, huku Wazayuni wakiwa wanavikodolea macho visima vya Qana vyenye utajiri mkubwa wa gesi ambayo ni mali ya Lebanon.Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, theluthi mbili ya visima hivyo ziko katika Kitalu nambari tisa cha Lebanon na theluthi moja ya mwisho iko chini kabisa ya mstari wa 23, yaani, katika eneo linalozozaniwa.
Akizungumza katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye toleo la leo la gazeti la Lebanon Al-Jumhoriya, kuhusu uhusiano na Hizbullah Aoun amesema: “tulilipa gharama ya uhusiano huu ambao ulikuwa ni kwa maslahi ya Lebanon; na Gebran Bassil, mkuu wa Harakati Huru ya Kitaifa ya Lebanon, naye pia aliadhibiwa na Wamarekani kwa sababu ya kuungana na Hizbullah na hatujuti kwa hilo; kwa sababu tulichofanya kilitokana na itikadi na imani yetu.”
Rais wa Lebanon amesisitiza kwa kusema, “Hizbullah ni moja ya viungo vya mwili wa taifa la Lebanon; tunaishi pamoja katika ardhi moja na tutabaki ndani yake humo pamoja; si pamoja na Waisraeli au Wamarekani au mtu mwingine yeyote. Kwa maneno mengine ni kwamba, kutokana na masuala ya wazi kabisa ya kitaifa na kimaadili na pasi na kujali maslahi yoyote ya kisiasa, inatulazimu tuwe bega kwa bega na washirika wetu katika kukabiliana na vitisho.”