Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema, misimamo ya Imamu Musa Sadr ni chemchemi ya ilhamu kwa Walebanon wote ili wafanye juhudi kwa ajili ya ukombozi wa nchi na watu wake.
Rais wa Lebanon ameyasema hayo kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyotekwa nyara Imamu Musa Sadr alipokuwa safarini nchini Libya.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya al Ahd, katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Aoun ameashiria kumbukumbu ya miaka 44 ya kutoweka Imam Musa Sadr baada ya kukutana na aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi nchini humo na kueleza: “miaka 44 imepita tangu kutekwa nyara Imam Musa Sadr, ilhali fikra zake na imani yake ingaliko Lebanon na njia yetu tunayofuata ni ya umoja”.
Rais wa Lebanon ameongezea kwa kusema: “ingawa katika hali hii ngumu Lebanon inakosa uwepo wa shakhsia huyu wa kitaifa na kiroho lakini misimamo yake ingali ni chemchemi inayotoa ilhamu na msukumo wa kufanya juhudi za kuiokoa Lebanon na watu wake.”
Mnamo tarehe 25 Agosti 1978 wakati Imam Musa Sadr alipokuwa katika awamu ya mwisho ya ziara yake ya kutembelea nchi kadhaa za Kiarabu, alielekea Libya kwa mwaliko rasmi wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo wakati huo Muammar Gaddafi, na akatekwa nyara na kutoweka tarehe 31 ya mwezi huo.
Tarehe 18 Septemba, na kufuatia maandamano ya upinzani ya wananchi wa Lebanon na malalamiko ya vyuo ya kidini na vyombo vya habari vya eneo, utawala wa Libya ulitoa taarifa na kutangaza kwamba Imam Musa Sadr na watu wawili alioandamana nao waliondoka Tripoli kuelekea Rome Italia Septemba 9 kwa ndege nambari 881 ya shirika la ndege la Alitalia. Kufuatia madai hayo, vyombo vya mahakama vya serikali za Lebanon na Italia, pamoja na uchunguzi uliofanywa na Vatican, kwa pamoja vilikanusha rasmi madai hayo ya Libya kwamba Sadr aliondoka nchini humo na kuwasili Rome; na hadi leo hii hatima ya shakhsia huyo mashuhuri wa Lebanon bado haijajulikana.