Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki dunia mapema Jumapili ya leo ikiwa ni wiki kadhaa tu baada ya kugunduliwa kuwa na saratani.
Ikulu ya Rais nchini Namibia imethibitisha habari ya kifo cha Rais wa nchi hiiyo na kueleza kuwa ni pigo kubwa kwa taifa hilo.
Hage Geingob, aliyekuwa na umri wa miaka 82, ameongoza taifa hilo la kusini mwa Afrika tangu 2015, mwaka ambao pia alitangaza kuwa alikuwa amepona saratani ya tezi dume.
Makamu wa Rais Nangolo Mbumba anachukua nafasi hiyo ya uongozi wa nchi hiyo yenye madini hadi uchaguzi wa rais na bunge utakapofanyika baadaye mwaka huu.
Ujumbe kutoka afisi ya rais uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X haukutoa taarifa yoyote kuhusu kilichosababisha kifo chake, lakini mwishoni mwa mwezi uliopita ilisema alisafiri hadi Marekani kwa ajili ya “matibabu ya siku mbili ya seli za saratani”, baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo kufuatia ukaguzi wa kawaida.
Geingob alizaliwa mwaka wa 1941 na baadaye kuwa mwanasiasa mashuhuri tangu kabla ya Namibia kupata uhuru kutoka kwa Afrika Kusini mwaka 1990.
Aliongoza jopo iliyotayarisha katiba ya Namibia, kisha akawa Waziri Mkuu wake wa kwanza baada ya uhuru mnamo Machi 21 mwaka huo, nafasi ambayo alishikilia hadi 2002.
Hage Geingob alifariki katika Hospitali ya Lady Pohamba huko Windhoek, ambako alikuwa akipokea matibabu kutoka kwa timu yake ya matibabu.
Wasiwasi kuhusu hali ya afya ya kiongozi huyo umekuwa ukiongezeka, huku ripoti zikieleza kwamba, alikiri mwaka jana kuwa afya yake ilikuwa imedhoofika. Geingob alitarajiwa kustaafu baadaye mwaka huu, baada ya kuhudumu kwa mihumla miwili kama rais.