Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza kuakhirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Februari 25, saa chache kabla ya kampeni rasmi kuanza.
Amri ya Novemba 2023 iliyotiwa saini na Sall iliweka tarehe ya uchaguzi huo wa rais kuwa Februari 25, huku wagombea 20 wakiwa katika kinyang’anyiro lakini viongozi wawili wakuu wa upinzani hawakujumuishwa.
Baada ya kutangaza kuwa hatagombea muhula wa tatu kama rais, Sall alimteua Waziri Mkuu Amadou Ba kutoka chama chake kuwa mrithi wake.
Baraza la Katiba limewaondoa baadhi ya wagombea kwenye kinyang’anyiro hicho, akiwemo kiongozi wa upinzani na mpinzani mkubwa wa mfumo tawala wa Senegal Ousmane Sonko, ambaye amefungwa jela tangu Julai 2023, na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani Abdoulaye Wade.
Wafuasi wa Wade katika Bunge la Taifa walitaka uchunguzi wa bunge ufanyike kuhusu upendeleo wa majaji wawili wa Mahakama ya Katiba, na hoja hiyo ilipitishwa na Bunge hilo Januari 31 na kuungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa chama cha Rais Sall pia…/