Rais wa Senegal amteua Ousmane Sonko kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo

Rais mmpya wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye amemteua Ousmane Sonko, kiongozi wa chama cha African Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity (PASTEF) kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hayo yalitangazwa jana Jumanne na Ikulu ya Rais huyo mpya.

Kwa hivi sasa Sonko, 49, ni meja wa jiji la Ziguinchor na ni kiongozi wa chama cha PASTEF ambacho kilivunjwa kwa amri ya rais Macky Sall mwezi Julai 2023.

Rais Faye, 44, aliapishwa mapema jana Jumanne katika mji wa Diamniadio ulioko umbali wa kilomita 30 kutoka Dakar, mji mkuu wa Senegal ili kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa miaka mitano ijayo.

Faye alishinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 24 Machi na kupata asilimia 54.28 ya kura.

Faye ni rais wa tano wa Senegal tangu nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilipopata uhuru wake kutoka kwa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa, mwaka 1960.

Zoezi la kuapishwa Diomaye Faye limefanyika baada ya Baraza la Katiba la Senegal kupasisha ushindi wa mgombea huyo wa kambi ya upinzani Ijumaa ya wiki iliyopita.

Katika taarifa yake ya siku hiyo ya Ijumaa, Baraza la Katiba la Senegal lilisema: “Kwa kuzingatia kuwa mgombea Bassirou Diomaye Diakhar Faye amepata kura 2,434,751, ambazo ni zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa… baraza hili linatangaza rasmi kuwa Bassirou Diomaye Diakhar Faye ndiye rais mteule.

Faye alifungwa jela mwezi Aprili 2023 na kuachiliwa Machi 14 mwaka huu baada ya kupitishwa sheria ya msamaha wa Rais aliyepita, Macky Sall.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *