Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ametangaza vita dhidi ya kundi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab ambalpo limekuwa likifanya mashambulio na mauaji mara kwa mara katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Rais huyo mpya wa Somalia ameahidi vita vikali vya kutokomeza kundi la al-Shabab katika taarifa yake ya kwanza kwa taifa tangu wanamgambo hao wafanye uvamizi mbaya kwenye hoteli moja mjini Mogadishu.
Shambulio hilo ambalo lilianza Ijumaa jioni, lilikuwa ndilo kubwa zaidi kuukumba mji mkuu wa Somalia tangu Rais Mohamud aingie madarakani mwezi Juni na kusisitiza changamoto ya kujaribu kumaliza uasi wa miaka 15 wa kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda.
Watu 21 walifariki na wengine 117 kujeruhiwa katika shambulio hilo lililolenga hoteli maarufu ya Hayat, na raia wa Norway ni miongoni mwa waliofariki dunia.
“Ninajua kwamba wananchi wa Somalia wamechoshwa na rambirambi na maombolezo yasiyoisha, najua kwamba mnawapoteza watu wenye thamani katika kila shambulio linolafanywa na magaidi,” Rais Mohamud amesema.
“Tuna dhamira ya kuwadhoofisha magaidi wanaoteketeza wanainchi wetu hadi maeneo yote wanayoyadhibiti yamekombolewa, hili ni jambo la kipaumbele kwa serikali yetu na maandalizi na utelekelezaji wa mpango huo unaendelea,” amesema bila kufafanua zaidi.
Genge la kigaidi la al-Shabab lilianzishwa mwaka 2004 na limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Genge hilo mara kwa mara limekuwa likishambulia wanajeshi wa serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika hasa katika mji mkuu Mogadishu na pia huwa linafanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia wa Somalia.