Rais Bashar al Assad wa Syria amesisitiza ulazima wa kupambana na misingi ya kifikra ya ugaidi na akaeleza kwamba, kupambana na ugaidi hakutawezekana kwa kutumia nguvu za kijeshi pekee, kwa sababu idiolojia ya mitazamo ya kufurutu ada haitambui mipaka bali inajipanua na kuenea kwa kasi kutoka nchi moja hadi nyingine.
Rais wa Syria ameyasema hayo katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Candith Mashego-Dlamini, ambapo pamoja na mambo mengine ametilia mkazo pia umuhimu wa kuwepo ushirikiano wa pamoja baina ya nchi mbalimbali kwa ajili ya kuleta amani na uthabiti.
Bashar al Assad amebainisha kuwa, dunia inazidi kuwa tata siku baada ya siku; na utata huo hautokani na suala la Ukarine kwa nafsi yake au matukio ya Syria, Yemen, Libya na maeneo mengine, bali ni kwa sababu athari za kiuchumi zinazosababishwa na matukio ya nchi hizo zinapelekea kukosekana uthabiti katika uga wa kimataifa.
Rais wa Syria amegusia pia ulazima wa kukabiliana na ugaidi na akaongezea kwa kusema, idiolojia ya ugaidi inaenezwa kwa njia ya intaneti na mitandao ya kijamii; na ukweli huo unatilia nguvu zaidi umuhimu wa kulipa uzito suala la kustawishwa mahusiano ya pande mbili baina ya nchi katika nyanja za kiuchumi na kiutamaduni.
Vilevile ameipongeza na kuisifu Afrika Kusini kwa mchango wake, ikiwa ni nchi yenye misimamo huru katika uga wa kimataifa na akaishukuru nchi hiyo kwa uungaji mkono wake kwa watu wa Syria katika vita vya kupambana na ugaidi na pia kwa kutetea haki za Syria za ardhi zake za miinuko ya Golan zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Bi Candith Mashego-Dlamini ameashiria kipindi kirefu cha misukosuko ya mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Apathaidi nchini Afrika Kusini na jinsi Syria ilivyowaunga mkono wananchi wa Afrika Kusini katika kipindi hicho na akabainisha kuwa, matukio yanayojiri hivi sasa nchini Syria yanahitaji ushirikishaji, majadiliano na kubadilishana mawazo kwa pamoja ili kupata njia ya kuutatua mgogoro uliopo.