Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amedai kuwa vitisho vya Iran vimevuka mipaka ya Asia Magharibi, na kueleza kwamba mbinu za kukabiliana na vitisho vya Tehran duniani inapasa zibadilishwe.
Macron, ambaye nchi yake ilichukua nafasi ya polisi mbaya katika mazungumzo ya awali ya kufikia makubaliano ya nyuklia na ya karibuni ya Vienna ya uondoaji vikwazo dhidi ya Iran, kwa mara nyingine tena amerudia madai yasiyo na msingi dhidi ya Tehran.
Katika mahojiano na chaneli ya televisheni ya Al-Hadath, rais wa Ufaransa amedai kuwa vitisho vya Iran vimevuka mipaka ya Asia Magharibi, na kueleza kwamba inapasa wabadilishe mbinu ya kukabiliana na vitisho vya Iran duniani.
Katika mahojiano hayo ambayo alifanyiwa siku ya Jumatano iliyopita kando ya mkutano wa mabadiliko ya tabaianchi uliofanyika Sharm al-Sheikh, Misri na kurushwa hewani jana Jumatatu na televisheni ya Al-Arabiya, Macron alidai kwamba: “lazima tuchukue hatua kwa uratibu ili kukabiliana na vitisho vya Iran”.
Huku akijaribu kuonyesha kuwa anawaunga mkono wananchi wa Iran dhidi ya vikwazo ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu, ambavyo lengo lake kuu ni kutoa mbinyo na mashinikizo kwa maisha na utafutaji riziki wa wananchi hao, Macron amedai kusema: “lazima tuhakikishe kuwa wananchi wa Iran hawaathiriwi na vikwazo hivyo.”
Kwa upande mwingine, msemaji wa serikali ya Ujerumani alitangaza jana Jumatatu kwamba wamo mbioni kutekeleza kifurushi cha vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.