Rais wa Uturuki aikosoa Marekani kwa kuunga mkono ugaidi Syria

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki amekosoa hatua ya Marekani ya kuyapa makundi ya kigaidi yaliyopo kaskazini mwa Syria msaada wa fedha na silaha.

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Erdogan akisema hayo na kuongeza kuwa, “Marekani inatuma malori 4,000-5,000 ya silaha na zana za kijeshi kaskazini mwa Syria. Ingawaje tumewaambia hili mara chungu nzima, lakini hawajali.”

Rais wa Uturuki amedai kuwa, “Tupo nanyi katika NATO, na ingawaje tuko pamoja (katika shirika hilo la kijeshi la Magharibi), lakini mnatukosea na mpo upande wa kundi la kigaidi.”

Hii ni katika hali ambayo, Uturuki imekuwa ikikosolewa na duru mbalimbali kwa kutuma wanajeshi wake kaskazini mwa Iraq na Syria, kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa PKK.

Serikali ya Damascus mara kwa mara imekuwa ikisisitiza kuwa, Marekani inapaswa kuondoa mara moja majeshi yake haramu kutoka Syria na kuacha kuwaunga mkono magaidi, mamluki na wanamgambo wanaotaka kujitenga; makundi ambayo inayatumia kufikia malengo yake.

Aidha Syria imekuwa ikikosoa pia vitendo vya askari wa Marekani kuiba mafuta na nafaka za nchi hiyo ya Kiarabu, kinyume na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mafuta ya Syria, vikosi vamizi vya Marekani pia vinaiba mapipa 66,000 za mafuta ghafi kwa siku katika nchi hiyo ya Kiarabu, sawa na asilimia 80 ya mafuta yanayozalishwa kwa siku nchini Syria.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *