Rais wa Vietnam ajiuzulu kutokana na makosa ya maafisa wake

Rais wa Vietnam ametangaza kujiuzulu kutokana na utepetevu na makosa yaliyofanywa na maafisa aliokuwa akiwasimamia, ikiwa ni chini ya miaka miwili baada ya kuchukua wadhifa huo.

Nguyen Xuan Phuc, 68, amewasilisha barua ya kujiuzulu, baada ya chama tawala cha Kikomunisti kumpata na hatia na kumbebesha dhima ya makosa yaliyofanywa na maafisa kadhaa wa serikali yake.

Shirika rasmi la habari la Vietnam limetangaza leo Jumanne kuwa, bado haijabainika ni nani atachukua nafasi iliyoachwa wazi na Xuan Phuc ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Kamati Kuu ya chama tawala imetangaza kuwa, “Huku akitambua wazi wajibu na majukumu yake mbele ya chama (tawala) na wananchi (wa Vietnam), (Nguyen Xuan Phuc) amejiuzulu na kustaafu.”

Kumekuwepo na tetesi kwa muda sasa za kujizulu Nguyen Xuan Phuc, hususan baada ya kufukuzwa kazi Manaibu 2 wa Waziri Mkuu, ambao walikuwa chini yake alipoiongoza serikali ya Vietnam.

Bunge la Taifa la Vietnam linatazamiwa kufanya kikao kisicho cha kawaida wiki hii, kwa ajili ya kuidhinisha hatua ya kujuzulu kwa rais huyo.

Vietnam haina mtawala mwenye mamlaka mutlaki, na kimsingi inaongozwa na mihimili minne mikuu; Katibu wa chama tawala, Rais, Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Bunge la Taifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *