Rais wa zamani wa Komoro Abdallah Sambi ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Rais wa zamani wa visiwa vya Komoro Abdallah Sambi amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la uhaini mkubwa.

Mahakama ya Usalama wa Taifa ya serikali ya Komoro ilitangaza jana wakati wa kusikilizwa kesi hiyo kwamba Ahmed Abdallah Sambi, rais wa zamani wa visiwa hivyo, ambaye alishtakiwa kwa uhaini, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Sambi alishtakiwa kwa kuuza pasipoti kwa watu wasio na utaifa wanaoishi katika nchi za Ghuba ya Uajemi.
Abdallah Sambi, mwenye umri wa miaka 64 na mpinzani mkubwa wa Rais Azali Osmani, ametiwa hatiani na Mahakama ya Usalama wa Taifa, chombo maalum cha mahakama ambacho maamuzi yake hayawezi kukatiwa rufaa.
Jaji wa mahakama hiyo Omar Bin Ali, alisoma hukumu dhidi ya rais huyo wa zamani wa Komoro akisema: Sambi amehukumiwa kifungo cha maisha jela. Mahakama inaamuru kutaifishwa mali na milki zake kwa manufaa ya Baitul-Mal.

Familia na wafuasi wa Sambi wamesema, mwenendo wa mahakama hiyo ni wa kisiasa na wamepinga hukumu iliyotolewa dhidi ya rais huyo wa zamani wa Komoro.

Ahmed Abdallah Sambi, ambaye aliongoza visiwa hivyo vidogo vya Bahari ya Hindi kati ya 2006 na 2011, alipitisha sheria mwaka 2008 iliyoruhusu uuzaji wa pasi za kusafiria kwa bei kubwa. Alituhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha katika mpango huo.
Komoro, ambayo ni majimui ya visiwa vitatu vilivyowahi kukoloniwa na Ufaransa vilivyoko kaskazini-magharibi mwa Msumbiji, imehimili miaka mingi ya machafuko ya kisiasa. Tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1975, nchi hiyo imeshuhudia majaribio ya mapinduzi zaidi ya 20, ambapo manne kati ya hayo yalifanikiwa.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *