Rais wa Zimbabwe atoa mwito wa kufanyika juhudi za kuhifadhi historia ya Afrika

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe jana Jumapili alizitaka nchi za Afrika kuhakikisha kwamba historia ya bara hilo imeandikwa kwa usahihi na kulindwa ili kuzuia dosari za kihistoria.

Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la Meidani ya Ukombozi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Jumba la Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika huko Harare, mji mkuu wa Zimbabe, Mnangagwa amesema kuwa, nchi yake itaendelea kuwekeza sana katika juhudi za kuandikwa upya historia ya bara la Afrika na kukabiliana na historia ya wakoloni iliyoandikwa ili kulinda maslahi ya wakoloni hao.

Mnangagwa amesema hayo katika sherehe zilizohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa nchi za SADC na kuongeza kwa kusema: “Tunafahamu kwamba historia ya bara letu imepotoshwa na inaendelea kupotoshwa makusudi ili kukidhi maslahi ya wakoloni wetu wa zamani.”

Jumba la Makumbusho la Ukombozi wa Afrika, ambalo bado linaendelea kujengwa mjini Harare, liko kwenye eneo la hekta 103 linalojulikana kama Jiji la Ukombozi.

Mnangagwa, ambaye alichukua uenyekiti wa SADC katika Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Jumamosi mjini Harare, amesema kuwa ni jukumu la kizazi cha hivi sasa kuhakikisha kuwa awamu muhimu katika historia ya Afrika inaandikwa kwa usahihi na kulindwa.

SADC, yenye makao yake makuu mjini Gaborone, Botswana, ni jumuiya ya kiserikali inayojumuisha nchi 16 wanachama ambazo ni Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kuisni, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *