Raisi: Iran inajitahidi kuwa na uhusiano wa pande mbili uliokita mizizi katika kuheshimiana na mataifa ya Afrika

Rais wa Iran Ebrahim Raisi anasema Tehran inataka kuwa na uhusiano na nchi za Kiafrika kwa kuzingatia msingi wa kuheshimiana na kufaidika, kinyume cha mataifa ya Magharibi ambayo yanataka tu kupora maliasili na utajiri wa Afrika.

Raisi aliyasema hayo katika mkutano wake wa Alhamisi na Rais mwenzake wa Senegal, Macky Sall kando ya mkutano wa 15 wa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi BRICS katika mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini.

“Tofauti na nchi za Magharibi, ambazo zinatazamia tu kupora rasilimali na utajiri wa nchi za Kiafrika, Iran inatafuta uhusiano unaozingatia heshima na manufaa ya pande zote mbili,” Raisi alisema.

Vile vile ameeleza utayarifu wa Iran kubadilishana maarifa, utaalamu, mafanikio na uwezo wake katika teknolojia, uhandisi, sayansi na viwanda na Senegal.

Kwa upande wake, Sall alipongeza mwaliko wa BRICS kwa Iran kujiunga na kundi hilo na kusema kuwa uwepo wa nchi hiyo katika umoja huo utasaidia kusawazisha mfumo wa kimataifa na kuunda ulimwengu wa pande nyingi.

“Nchi za Magharibi, kama wavunjaji wakuu wa haki za binadamu, zinataka kuweka shinikizo kwa nchi zenye misimamo huru chini kisingizio cha eti kutetea haki za binadamu,” rais wa Senegal alisema.

Aidha alisisitiza kuwa, nchi ambazo kwa karne nyingi zimekuwa zikifanya utumwa kwa kiwango kikubwa na zina rekodi  mbaya ya ukoloni, na hata siku hizi zinaendelea na sera kama hizo kwa njia zingine hazina haki ya kudai kuwa watetezi wa haki za binadamu.

Akiwasilisha shauku yake ya kutaka ushirikishwaji zaidi wa makampuni na wafanyabiashara wa Iran nchini Senegal, Sall amesisitiza kuwa, taifa hilo la Afrika Magharibi linataka kutumia utaalamu wa Iran na kustawisha ushirikiano uliopanuliwa katika nyanja za nishati na sayansi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *