Raisi: Kuuawa shahidi kidhulma Imam Hussein (AS) kunathibitisha umuhimu mkubwa wa kuamrisha mema na kukataza maovu katika dini ya Uislamu

Rais Ebrahim Raisi amesema, kuuawa shahidi kidhulma Imam Hussein (AS) ni ithibati kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu kuna umuhimu mkubwa katika dini ya Uislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mkutano na wajumbe wa tume ya kuhuisha uamrishaji mema na ukatazaji mabaya.

Katika mkutano huo na wajumbe hao, Seyyid Ebrahim Raisi amegusia kufanyika kikao hicho wakati mmoja na kuanza kwa siku za maombolezo ya Muharram na akasema, Imam Hussein (AS) ni mbeba bendera wa faradhi hiyo muhimu ya dini.

Amefafanua kuwa, harakati adhimu ya Aba Abdillahil-Hussein (AS) na kuuawa kwake shahidi kidhulma ni ithibati kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu kuna umuhimu mkubwa katika dini ya Uislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuzingatiwa uwezo mkubwa wa watu nchini na jumuiya za wananchi kwa ajili ya kuhuisha faradhi ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

Katika mkutano huo, wajumbe kadhaa wa tume ya kuamrisha mema na kukataza mabaya walihutubia kabla ya Rais Raisi na kutoa mapendekezo kadhaa ya kufanyiwa kazi kwa ajili ya kufanikisha faradhi muhimu ya kuamrisha mema na kukataza mabaya katika jamii.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa, ni pamoja na kuanzishwa shura za kuamrisha mema na kukataza mabaya katika vyombo vya serikali, kutekelezwa sheria ya kuwahami waamrishaji mema na wakatazaji maovu, kukabiliana na madhara ya intaneti na maadili machafu yaliyoratibiwa katika uga wa utamaduni na kuimarisha asasi za wananchi katika kuhuisha faradhi ya kuamrisha mema na kukataza mabaya .

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *