Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa Iran na Syria ni thabiti na kwamba umejengwa katika misingi ya moyo wa muqawama na mapambano ya wananchi wa mataifa haya mawili.
Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumanne hapa Tehran katika mazungumzo yake na Ali Mahmoud Abbas, Waziri wa Ulinzi wa Syria na kusisitiza kuwa, Tehran itaendelea kushirikiana na serikali halali ya Syria.
Amesema taifa la Iran ni rafiki wa dhati wa serikali na taifa la Syria, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono kwa dhati wananchi, serikali, jeshi na kambi ya muqawama huko Syria.
Rais wa Iran amesema himaya ya Tehran kwa serikali ya Syria katika kipindi chote cha mgogoro na msaada wake kwa nchi hiyo katika kupambana na makundi mbalimbali ya kigaidi ni ushahidi na ithibati ya taifa hili kushirikiana na nchi hiyo ya Kiarabu.
Amesema kama ambavyo wananchi wa Iran walisimama kidete kuwatetea, kuwahami na kuwasaidia wananchi wa Syria wakati wa matatizo, vivyo hivyo pia ipo tarayi kushiriki katika kulikarabati na kulijenga upya taifa hilo.
Kwa upande wake, Ali Mahmoud Abbas, Waziri wa Ulinzi wa Syria amesema wananchi wa Syria waliibuka washindi katika vita dhidi ya ugaidi kutokana na uungaji mkono wa ndugu na marafiki zao wa kweli wa Iran.
Amesema kambi ya muqawama itakuwa na nafasi na jukumu kubwa ya kuifinyanga dunia mpya. Waziri wa Ulinzi wa Syria ameongeza kwa kusema, “Maadui daima wamekuwa wakila njama za kuvuruga uhusiano wa Iran na Syria, lakini uhusiano wa nchi mbili hizi umekita mizizi na hauwezi kutetereshwa na njama hizo.”