Rais wa Afrika Kusini amesema kwamba amefurahishwa na jinsi timu ya wanasheria wa nchi yake ilivyojadili kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kwamba ni fakhari kwa nchi yake kufungua kesi hiyo dhidi ya Israel.
Rais Cyril Ramaphosa amesema hayo wakati akihutubia Umoja wa Wanawake wa chama chake cha African National Congress (ANC) na kusema kwa kujiamini kwamba: “Sijawahi kupata hisia hizi za fakhari kama nilizopata wakati timu yetu ilipokuwa ikijadili kesi yetu (dhidi ya Israel) huko The Hague.”
Amesema nchi yake imeweka timu madhubuti ya wanasheria kuwakilisha kesi ya Afrika Kusini katika mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa huko The Hague, Uholanzi.
Afrika Kusini iliwasilisha kesi yake katika Mahakama ya ICJ mwezi uliopita wa Disemba 2023, kutokana na Israel kukanyaga Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948. Iliwasilisha hati ya kurasa 84 na mahakama ikielezea vitendo inachosema ni sawa na mauaji ya kimbari huko Gaza.
Mahakama ya ICJ ilisikiliza hoja za Afrika Kusini jana Alkhamisi zilizowasilishwa kwenye hati ya kurafa 84 na leo Ijumaa imesikiliza majibu ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa upande wao Wapalestina walikusanyika Jumatano katika uwanja wa Nelson Mandela huko Ramallah ili kuishukuru Afrika Kusini kwa hatua yake ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Washiriki katika mkusanyiko huo walibeba mabango yenye maandishi yanayotaka kukomeshwa vita haraka iwezekanavyo huko Ukanda wa Ghaza.
Ikumbukwe kuwa shujaa Nelson Mandela alikuwa anasisitiza mara kwa mara kwamba hali mbaya na masaibu waliyo nayo Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza na wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ni sawa na waliyopitia raia weusi wa Afrika Kusini wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi na muda wote walikuwa yuko pamoja na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.