Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametangaza kuwa, uchaguzi wa urais na wa Wabunge wa nchi hiyo utafanyika tarehe 14 Mei mwaka huu.
Erdogan ametoa tangazo hilo jana kwa kusema: “Ninatumia mamlaka yangu kutangaza kuwa, uchaguzi wa rais na ule wa Bunge utafanyika tarehe 14 Mei mwaka huu.
Akizungumza na vijana wanaotarajiwa kupiga kura kwa mara ya kwanza, Erdogan amesema: Ninawataka wawakilishi wetu vijana ambao watashiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza baada ya kutimiza sharti la umri, wajitokeze katika uchaguzi wa tarehe 14 Mei na kuchagua chaguo sahihi.
Uchaguzi huo awali ulipangwa kufanyikka Juni 18 mwaka huu.
Hii ni katika hali ambayo, Jumatato iliyopita, Rais wa Uturuki aliashiria juu ya uwezekano wa uchaguzi huo kufanyika mapema.
Uchaguzi wa Rais na Bunge ambao unafanyika kwa pamoja unahesabiwa kuwa mtihani mkubwa kwa Rais Erdogan hasa kutokana na changamoto mbaliimbali ambazo zinaikabili nchi hiyo kwa sasa hasa suala la uchumi.
Tangazo hilo la kufanyika uchaguzi Mei 14 limezua maswali mengi ya kisheria na kuibua mijadala mikali kati ya wataalamu na wawakilishi mbalimbali wa kisiasa nchini Uturuki.
Erdogan mwenye umri wa miaka 68 na ambaye amekuwa Rais wa nchi tangu mwaka 2014 anatarajiwa kutetea kiti chake katika uchaguzi huo wa Mei.
Wapinzani wa Erdogan wanakosoa vikali sera zake za kiuchumi huku tafiti mbalimbali za maoni zikionyesha kupungua uungaji mkono na kuporomoka kupendwa kiongozi huyo nchini Uturuki.