Historia ya soka iliwekwa siku ya Jumamosi, wakati kadi nyeupe, ambayo inatumika kuthamini moyo wa kimichezo ilipoonyeshwa kwa mara ya kwanza katika mechi ya ligi nchini Ureno.
Wakati kadi za njano na nyekundu zimekuwa zikitumika kwa miongo kadhaa kutoa adhabu kwa wachezaji, shirikisho la soka la Ureno hivi majuzi lilianzisha utoaji kadi nyeupe ili kuwapa waamuzi fursa ya kuwazawadia wale wanaoonyesha moyo wa kimichezo.
Mwamuzi Catarina Campos alionyesha kadi hiyo nyeupe kutambua na kuhimiza moyo wa kimichezo katika pambano la mechi za wanawake za ligi ya Ureno kati ya Sporting Lisbon na Benfica iliyochezwa mjini Lisbon mwishoni mwa juma.
Karibu na kumalizika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo, ambapo Benfica ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0, mtu mmoja aliugua ghafla kwenye eneo la kando ya uwanja ambapo timu za madaktari wa klabu zote mbili walikimbilia kutoa msaada na kitendo hicho ndicho kilichomfanya mwamuzi kuonyesha kadi nyeupe kwa timu zote mbili ikiwa ni kuthamini moyo wa kimichezo na kimaadili ulioonyeshwa na kada hizo za tiba.
Hatua hiyo ya wahudumu wa tiba na uamuzi wa refa Campos kuwazawadia kadi nyeupe viliwafanya mashabiki na watazamaji katika uwanja wa michezo wa Estadio da Luz wapige makofi.
Katika mechi hiyo Benfica ilishinda mabao 5-0.