Rekodi Mpya ya Wakimbizi Duniani

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu idadi kubwa na isiyo na kifani ya wakimbizi katika ripoti ambayo imepewa anwani “Mashtaka Dhidi ya Hali ya Sasa ya Dunia.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takriban watu milioni 110 duniani kote wamelazimika kuacha nyumba na maeneo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vita na migogoro ya ndani.

Katika mazingira ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya hivi sasa nchini Sudan, familia nyingi zimelazimika kuacha nyumba na makazi yao, jambo ambalo lilikuwa tayari limesababisha matatizo makubwa kutokana na vita kati ya Russia na Ukraine, pamoja na hali ya Afghanistan. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema katika ripoti yake ya mwaka kwamba idadi ya wakimbizi wanaokimbia nchi na makazi yao au watu waliolazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao haijawahi kuwa kubwa kwa kiwango kinachoshuhudiwa hivi sasa. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, idadi ya wakimbizi au wanaotafuta hifadhi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana (2022) ilikuwa watu milioni 108 na laki 4. Idadi hii imeongezeka kwa watu milioni 19 na laki moja ikilinganishwa na takwimu zilizotayarishwa kuhusu idadi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi duniani mwishoni mwa 2021, suala ambalo linaonyesha ongezeko kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya pande mbili zinazohasimiana nchini Sudan vimezidisha idadi ya wakimbizi na kufikia karibu milioni 110 mwezi Mei mwaka huu. Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Geneva, Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, ameelezea masikitiko yake makubwa kutokana na ongezeko la idadi ya wakimbizi ikilinganishwa na mwaka jana, na kusema: “Tuna watu milioni 110 ambao “wamekimbia makazi yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo migogoro, manyanyaso, ubaguzi na ukatili ambao mara nyingi huchanganyika na mambo mengine hasa athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.”

Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, jumla ya watu milioni 35 na laki tatu wanaotafuta hifadhi na wakimbizi milioni 62 na laki tano walisajiliwa mwaka 2022 pekee. Wakimbizi na watafuta hifadhi milioni kumi na laki sita miongoni mwao wametajwa kuwa wanahitajia sana himaya na misaada ya kimataifa. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi amesema watu hawa wote wanakabiliwa na “mazingira ya uadui mkubwa zaidi” karibu kila mahali wanakokwenda kutafuta hifadhi. Filippo Grandi amesisitiza haja ya kurekebishwa sera zinazohusiana na wakimbizi, na kutoa wito wa kufunguliwa milango kwa wanaotafuta hifadhi huko Ulaya, Uingereza na Marekani.

Wakati huo huo, Grandi ameashiria mpango wa serikali ya Uingereza wa kutuma wahamiaji nchini Rwanda na kusema watafuta hifadhi hawapaswi kuwekwa gerezani, akisisitiza kuwa “kuomba hifadhi sio uhalifu.” Pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu sera za uhamiaji za Marekani na mashinikizo ya nchi hiyo dhidi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi.

Katika upande mwingine Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi amesema kuwa shirika hilo chini ya uongozi wake, kama yalivyo mashirika mengine mengi ya masuala ya kibinadamu kama vile Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, mwaka huu halina hali nzuri ya kifedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji kutokana na hali ngumu ya uchumi wa dunia na mfumuko wa bei. Ripoti hiyo imezitaja Uturuki (yenye wakimbizi milioni 3.6), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (iliyopokea wakimbizi milioni 3.4), Colombia (iliyo na wakimbizi milioni 2.5), Ujerumani (yenye wakimbizi milioni 2.1) na Pakistani (wakimbizi milioni 1.7) kuwa ndizo nchi zilizotoa hifadhi kwa idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu ongezeko lisilo na kifani la idadi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi duniani, imetolewa huku jamii ya kimataifa, hasa nchi za Ulaya na Marekani, ambazo ndio kimbilio kuu la wakimbizi hao, zikipuuza mahitaji yao muhimu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za Magharibi kurekebisha sera zao za uhamiaji na kupitia upya masharti magumu kuhusu wanaotafuta hifadhi.

Ikumbukwe kwamba vipengele mbalimbali vya mikataba na hata Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu vinasisitiza ulazima wa serikali na nchi kutilia maanani suala la wakimbizi. Kwa hiyo, ni wajibu wa serikali zote kutosita kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi na kutimiza wajibu wao wa kibinadamu. Mojawapo ya vifungu vya Azimio la Milenia la Umoja wa Mataifa lililoidhinishwa mwaka 2000 kuhusu ulinzi wa watu walio katika mazingira magumu, kinasisitiza kwamba jitihada zinapaswa kufanywa ili kupunguza mateso ya wanadamu na kuwapa msaada na usaidizi wa aina yoyote ambao ni muhimu ili waishi maisha ya kawaida, na kulinda usalama na hadhi yao ya kibinadamu.

Kifungu cha 14 cha Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu la mwaka 1948 kinawapa wakimbizi haki ya kutafuta hifadhi katika nchi nyingine kutokana na hatari mbalimbali wanazokabiliana nazo. Kadhalika, Kifungu cha 11 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni wa mwaka 1966 kinaelekeza kuwa, nchi zote wanachama wa mkataba huo zimejitolea kutoa chakula na makazi ya kutosha ili kuboresha hali ya raia. Hili ndilo lengo kuu la “Tamko la Mkutano wa Dunia wa 1996 wa Istanbul juu ya Makazi ya Kibinadamu”. Kifungu cha tano cha tamko la Mkutano wa Dunia wa Makazi wa Istanbul 1996 kinasisitiza kwamba, kuwapa makazi binadamu ni mchakato wa kimataifa, na nchi zinalazimika zikubali ukweli kwamba wahamiaji na wakimbizi ni miongoni mwa watu walio katika mazingira magumu ambao yumkini pia wanasumbuliwa na umaskini; na kupuuzwa kwa watu waliopatwa na maafa walioko ng’ambo ya nyaya za mpakani wakiingojea kesho yao kwa wasiwasi, sio kitendo cha kiadilifu wala cha kibinadamu.

Kuhusu hali ya wakimbizi na waomba hifadhi, kunajitokeza swali kwamba ni kitu gani kinachowalazimisha baadhi ya watu kuondoka katika nchi na maeneo yao na kutafuta maeneo mapya kwa ajili ya kuendelea na maisha yao?

Vita vya wenyewe kwa wenyewe, uvamizi wa madola ya kigeni, matatizo ya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na njaa, matatizo yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama ukame, mafuriko na kadhalika, pamoja na kutafuta maisha bora, ni miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya watu wakimbie na kuhama makazi na nchi zao za asili. Pamoja na hayo katika miongo miwili iliyopita siasa za kivita za nchi za Magharibi ikiwemo Marekani katika eneo la Asia Magharibi zimekuwa miongoni mwa mambo ambayo yamezidisha wimbi la wakimbizi kutoka baadhi ya nchi za eneo hilo zikiwemo Syria na Afghanistan kuelekea maeneo mengine ya dunia.

“George Mastakis”, Profesa wa Sosholojia na mtaalamu wa masuala ya kidini na kijamii wa Ugiriki, amezungumzia matatizo ya wahamiaji na sababu ya zilizowalazimisha kuelekea Ugiriki na nchi nyingine za Ulaya, akisema: “Sera za kuchochea vita za nchi za Magharibi katika nchi za Kiislamu zimelazimisha idadi kubwa ya raia wa eneo la Mashariki ya Kati kuondoka makwao na kutafuta hifadhi katika nchi kama vile Ugiriki.” Pofesa huyo anasisitiza kuwa njia pekee ya kusitisha wimbi hilo la wahajiri ni kukomeshwa vita vya nchi za Magharibi katika nchi mbalimbali na kuyapokonya silaha makundi ya kigaidi. Ameongeza kuwa: Nchi za Magharibi zinapaswa kuacha kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kuwaacha watu wa nchi za Mashariki ya Kati waamue kwa uhuru mustakbali wao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *