Harakati ya “kuziba midomo” iliyofanywa na wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Ujerumani kwenye mechi yao ya ufunguzi katika Kombe la Dunia 2022 huko Qatar dhidi ya Japan, ilisababisha matatizo ndani ya kambi ya timu hiyo, na kuibua tofauti kati ya wachezaji ambao walikataa kushiriki kwenye kampeni ya kutetea ushoga.
Harakati hiyo ya kuziba midomo ya wachezaji wa timu ya soka ya Ujerumani ilichukuliwa dhidi ya uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) wa kukataza kuvaa beji zinazowatetea mashoga wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar.
Uamuzi wa maafisa wa timu ya soka ya Ujerumani wa kutetea vitendo vichafu vya ushoga na ubaradhuli umekosolewa sana na wachezaji wa soka wa timu nyingine hata wa Ujerumani wenyewe. Miongoni mwa wanasoka mashuhuri waliolaani harakati hiyo ni nahodha wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Eden Hazard, ambaye alisema kwamba: “Timu ya taifa ya Ujerumani ilipaswa kuzingatia kucheza mpira, na sio kutuma ujumbe wa kisiasa.”
Tovuti ya Fox Sports imetangaza kwamba habari zilizovuja kutoka ndani ya kambi ya timu ya kitaifa ya Ujerumani baada ya kubanjuliwa katika mashindano ya Kombe la Dunia mapema huko Qatar zimefichua kuwa kulitokea mgawanyiko mkubwa kati ya wachezaji wa timu hiyo, ambao uliathiri mazingira kwa ujumla ndani ya timu ya soka ya Ujerumani, na – kwa kiwango kikubwa – ulisababishwa kuondolewa mapema timu hiyo, licha ya kuingia kwenye mashindano hayo ikitambuliwa kuwa ni miongoni mwa timu zinazotazamiwa kushinda Kombe la Dunia.
Tovuti hiyo imenukuu vyanzo vya karibu na timu ya taifa ya Ujerumani vikithibitisha kwamba “hakukuwa na makubaliano kati ya wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani kuhusu harakati hiyo ya kutetea ushoga.”
Ripoti hiyo imesema: “Tofauti na kile Chama cha Soka cha Ujerumani kilijaribu kuonyesha kikidai kwamba harakati hiyo iliungwa mkono na wachezaji wote, ukweli ulikuwa tofauti kabisa.”
Chanzo kimesisitiza kwamba “baadhi ya wachezaji waliona kuwa walikuwa wakitumiwa vibaya kushiriki katika kampeni hiyo, licha ya kwamba inapingana na imani zao.”
Ripoti zinasema kulitokea ugomvi kati ya kikundi cha wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani hata kabla ya kuingia uwanjani ili kukabiliana na timu ya taifa ya Japan ambayo iliichapa mabao mawili kwa moja.
Timu ya taifa ya Ujerumani ilishambuliwa vikali kwa dhihaka kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya kijamii kote duniani kutokana na kujihusisha na masuala ya kutetea ushoga badala ya kazi yake ya mpira wa miguu, jambo ambalo lilizidisha mashinikizo kwa timu hiyo na kuwa miongoni mwa sababu za kuondolewa haraka kwenye mashindano hayo.