Ripoti kuhusu jinai za kivita za muungano wa Saudia na Imarati nchini Yemen

Kituo cha sheria cha Ain al-Insaniyah (Jicho la Ubinadamu) cha Yemen kimetoa takwimu za kushtua kuhusu maafa ya kibinadamu na kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia na Imarati katika nchi hiyo, takwimu ambazo zinaanika wazi wigo wa jinai za kivita zilizofanywa na muungano huo na waungaji mkono wake wa Magharibi na Wazayuni.

Mbali na kuwa jinai hizo za kutisha zinatilia shaka madai ya eti kutetea haki za binadamu yanayotolewa na mashirika ya kimataifa katika uwanja huo, suala hilo hilo pia linaanika wazi uzembe unaofanywa na taasisi za kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa katika kuuwajibisha muungano huo wa Saudia na Imarati pamoja na waungaji mkono wao wa Magharibi na Wazayuni kuhusu jinai hizo za kutisha zinazotekelezwa dhidi ya watu wa Yemen wasio na hatia.

Kwa mujibu wa ripoti ya maandishi ya kituo hicho cha sheria cha Yemen, katika siku 2,800 za vita, Wayemeni elfu 18,013 waliuawa shahidi na wengine elfu 29, 660 kujeruhiwa, ambapo kati ya hao watoto 4,061 waliuawa shahidi na 4,739  walijeruhiwa. Wanawake 2,454. waliuawa shahidi na waengine 2,966 kujeruhiwa katika vita hivyo vya kichokozi.

Pia katika kipindi hicho, nyumba 598, 737 za makazi, vyuo vikuu 182, misikiti 1,679, vituo vya utalii 379, hospitali na vituo vya afya 415, shule na vituo vya elimu 1,242, viwanja vya michezo 140, Maeneo ya kihistoria 255, vituo vya habari na utangazaji 61, ardhi za kilimo 10, 803, viwanja vya ndege 15, bandari 16, mitambo ya kuzalisha umeme 344, barabara na madaraja 7,099, mitandao na vituo vya mawasiliano 616, hifadhi na mabomba ya maji 2,974 miundombinu ya kiserikali 2,101, viwanda 407, meli za mafuta 385, majengo ya biashara 12,030, vituo 454 vya mifugo na kuku, magari madogo 10,112, malori ya kubeba chakula 998,  masoko 700, boti za uvuvi 485, maghala  ya chakula 1,014 na vituo  425 vya kujazia mafuta ya petroli na dizeli kwenye magari vilishambuliwa na kuharibiwa kabisa katika vita hivyo vya muungano wa kivamizi wa Saudi Arabia.

Kwa takwimu hizi za kushtua, ni wazi kwamba stratijia ya muungano huo vamizi ilikuwa na ingali ni kuiharibu kabisa Yemen na kuisawazisha na ardhi.

Jambo muhimu na la kuzingatia katika ripoti ya maandishi ya kituo cha sheria cha Ain al-Insaniyah cha Yemen, ambayo imeelezea kwa kina uharibifu uliofanyika katika maeneo yaliyoshambuliwa, ni kwamba hakuna shabaha muhimu za kijeshi zilizolengwa katika jinai hiyo bali sehemu kubwa ya waliopoteza maisha ni raia wa kawaida na sehemu kubwa ya uharibifu uliofanywa pia ni maeneo na vituo vya kiraia, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa muungano huo wa kijeshi tangu mwanzo haukuwa na lengo jingine isipokuwa kuiangamiza Yemen na kuwafukuza wenyeji wa nchi hiyo kutoka kwenye ardhi yao, ili kuupa fursa ya kuigawanya Yemen kati ya wanachama wa muungano huo wa kichokozi.

Ingawa muungano huo ulianzisha vita dhidi ya Yemen kwa madai ya kuunga mkono serikali iliyojiuzulu ya Abd Rabu Mansour Hadi, lakini baada ya kupita muda ilibainika wazi kuwa muungano huo na waungaji mkono wake wa Magharibi na Wazayuni ulikuwa na mpango ulioainishwa awali wa kuigawa Yemen kwa msingi wa maslahi ya wanachama wake na hasa Saudia na Imarati. Mpango huo ulikusudiwa kuipa Imarati fursa ya kudhibiti na kukalia kwa mabavu bandari na visiwa vya kistratijia vya Yemen nayo Saudi Arabia iweze kuunganisha majimbo kama Hadhratmaut na ardhi yake ili kwa njia hiyo ifanikiwe kuchimba mifereji ya kupitishia mabomba yake ya mafuta kuelekea Bahari ya Arabia na hivyo kupunguza utegemezi wake kwa Ghuba ya Uajemi.

Kutekelezwa mpango wa kutaka kuikaliwa Yemen kwa mabavu, ambao ni sawa na kubuniwa Palestina nyingine katika eneo, bila shaka kutapelekea mamilioni ya Wayemen wengine wasio na hatia kutumbikia kwenye njama kubwa zaidi ambayo sehemu ndogo ya madhara yake yametajwa katika ripoti ya karibuni ya kituo cha Yemen cha Ain al-Insaniya.

Hii ni kwa sababu hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen zimewafanya mamilioni ya watu kuyahama makaazi yao na kuwaweka mamilioni ya wengine kwenye ukingo wa baa la njaa, jambo ambalo mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakionya mara kwa mara juu  ya madhara yake. Kwa miongo kadhaa iliyopita rasilimali za mafuta na gesi na vile vile maliasili nyingine za nchi hiyo masikini zimekuwa zikitazamwa kwa jicho la tamaa na serikali za Saudia na Imarati pamoja na waungaji mkono wao wa Magharibi. Ni kwa msingi huo, ndipo serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen inayoongozwa na mrengo wa Ansarullah, ikasisitiza kuwa katika mpango wowote wa amani, wahanga wa vita vya Yemen wanapaswa kulipwa fidia na miundo msingi pamoja na vituo vyote vilivyoharibiwa kujengwa upya na wale walioviharibu.

Kusimamishwa kabisa ukaliwaji wa Yemen ni moja ya masharti mengine yanayosisitizwa na Wayemeni, na hii ina maana kwamba serikali za Saudia na Imarati zinapaswa kuwajibishwa na kulazimishwa kuchukua hatua zinazofaa katika uwanja huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *