Elizabeth II, Malkia wa Uingereza aliyefariki dunia siku chache zilizopita alikuwa akitambuliwa na watu wengu kuwa ni nembo utawala wa kikoloni.
Malkia Elizabeth II wa Uingereza alifariki dunia Alhamisi jioni akiwa na umri wa miaka 96.
Kifo cha Elizabeth II na utawala wake wa muda mrefu wa miaka 70 kuanzia 1952 hadi 2022, ambao nusu yake ulikuwa wakati wa mapambano ya mataifa mbalimbali dhidi ya ukoloni wa Uingereza na harakati za kupigania kujikomboa kutoka kwenye makucha ya utawala wa London, ni ukumbusho wa urithi wa ukoloni wa Uingereza duniani, ambao umeendelea kwa mamia kadhaa ya miaka.
Moses Ebe Ochonu, profesa wa utafiti wa masuala ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Vanderbilt nchini Marekani, amesema kwamba kifo cha Malkia Elizabeth kimewaelekeza tena wanaadamu kwenye utawala wake wa kikoloni na kuongeza kuwa: “Uingereza haijawahi kuwajibika kikamilifu kutokana na jinai na uhalifu wake.”
Akiashiria kwamba Elizabeth II alikuwa nembo ya Uingereza ya kukana uhalifu uliofanywa na nchi hiyo katika kipindi cha ukoloni, Ebe Ochonu amesema: “Nchini Nigeria na Kenya pekee, maelfu ya wapigania uhuru waliteswa na serikali ya kikoloni ya Uingereza.”
Opal Palmer Adisa ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa Taasisi ya Jinsia na Maendeleo katika Chuo Kikuu cha West Indies, Jamaica, pia amesema: “Uingereza hata haijawaomba msamaha Waafrika waliohamishwa kwa mabavu kutoka katika nchi zao na kuuzwa kama watumwa.”
Palmer Adisa amesema, zaidi ya watumwa milioni 2.2 walisafirishwa na kupelekwa katika makoloni ya Uingereza katika Bahari ya Karibi.
Palmer Adisa amesisitiza kuwa, hadi sasa, watoto hawajapewa taarifa sahihi na makini kuhusu kile kilichotokea wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza hususan kipindi cha utumwa.
Chama cha The Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini pia kimetangaza kuwa hakiombolezi kifo cha Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.
Taarifa ya EFF imesema: “Hatuombolezi kifo cha Elizabeth, kwa sababu kwetu kifo chake ni ukumbusho wa kipindi cha kutisha sana Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.”
Taarifa hiyo imekumbusha jinai zilizofanywa na utawala wa kikoloni wa Uingereza nchini Afrika Kusini ambapo utajiri ulioporwa nchini humo ulitajirisha familia ya kifalme ya Uingereza.
EFF imeongeza kuwa ni familia ya kifalme ya Uingereza iliyoidhinisha vitendo vya Cecil John Rhodes, kupora utajiri Zimbabwe na Zambia. Aidha chama hicho cha mrengo wa kushoto Afrika Kusini kimesema ilikuwa ni familia ya kifalme ya Uingereza iliyofaidika na mateso na ukatili dhidi wa watu wa Kenya waliokuwa wakipambana kishujaa dhidi ya ukoloni wa kijinai wa Uingereza.