Ripoti zilizochapishwa kuhusu hali ya ukame duniani mwaka 2022 zinaonesha kuwa hali ya kutisha kuhusu ukosefu wa maji na mazao ya kilimo itaendelea katika miaka ijayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), ripoti na takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa, mwaka 2022 ulitajwa kuwa mwaka wa ukame zaidi duniani katika miongo michache iliyopita, wakati nchi nyingi za dunia katika mabara tofauti zikikabiliwa na ukame na uhaba wa mazao ya kilimo.
Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu zilitangaza katika ripoti ya pamoja iliyotolewa Oktoba 2022 kwamba baadhi ya maeneo ya Afrika na Asia hayatakuwa tena mahala pa kuishi wanaadamu kutokana na joto kali ndani ya miongo michache ijayo.
Katika bara la Asia, nchi za India na Pakistan zilikabiliwa na ukame zaidi ya nchi zingine za bara hilo, kiasi kwamba mwezi Machi mwaka huu, joto kali liliua watu 90 katika nchi hizo.
Katika bara la Afrika, joto kali na ukame vimezifanya nchi nyingi za bara hilo zikabiliwe na njaa isiyo na kifani.
Mnamo Agosti 2022, Tume ya Ulaya pia ilichapisha ripoti juu ya hali mbaya ya ukame katika nchi za bara hilo. Ripoti hiyo imesema kuwa mwaka uliomalizika jana wa 2022 Ulaya ilikabiliwa na ukame mbaya zaidi ambao haujawahi kushuhudiwa katika miaka isiyopungua 500.
Katika mwaka uliomalizika jana wa 2022, sehemu nyingi za Amerika Kaskazini pia zilikabiliwa na ukame mkali, ambao ulisababisha moto wa nyika katika majimbo ya Arizona, Colorado, California, Oregon, na Washington.