Russia: Hakuna ushahidi Iran inataka kuunda silaha za nyuklia

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema hakuna ithibati wala ushahidi wowote unaoashiria kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuzalisha silaha za nyuklia au kutazama upya uanachama wake katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT.

Vladimir Yermakov, Mkurugenzi wa Idara ya Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia na Kudhibiti Silaha katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia amesema hayo na kuongeza kuwa, Iran daima imekuwa mshiriki amilifu na mwanachama wa NPT.

Yermakov amenukuliwa na shirika la habari la Sputnik akieleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasalia kuwa nchi mwanachama wa Mkataba wa NPT iliyokaguliwa mara nyingi zaidi, na katika kaguzi zote hizo, hakuna kitu kilichoashiria kuwa Iran imekengeuka wajibu wake.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameeleza bayana kuwa, “Hakuna ushahidi unaoonesha kuwa Tehran ina azma ya kutathmini upya majukumu yake katika Mkataba wa NPT, kwa shabaha ya kuzalisha silaha za nyuklia.”

Licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuthibitisha katika ripoti zake kadhaa kuwa mradi wa nyuklia wa Iran una malengo ya amani na kiraia, lakini viongozi wa Kizayuni na Marekani wamekuwa wakieneza propganda kwamba Tehran inataka kuzalisha silaha za maangamizi za atomiki.

Ifahamike kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio utawala pekee ambao si mwanachama wa NPT katika eneo la Asia Magharibi licha ya kujilimbikizia vichwa vya silaha hatari za mauaji ya halaiki ya watu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *