Russia kuipa Iran idadi kubwa ya ndege za kivita za kisasa aina ya Sukhoi Su-35

Hivi karibuni Russia inatazamiwa kuipatia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndege za kivita aina ya Sukhoi Su-35 hatua ambayo yumkini ikazikasirisha zaidi nchi za Magharibi kutokana na ushirikiano wa kijeshi unaozidi kuimarika kati ya Tehran na Moscow.

Ripoti za vyombo vya habari, zikiwanukuu wataalamu wa kijeshi, Iran itapokea ndege 24 za kivita za Sukhoi Su-35 . Ndege hii ya kisasa kabisa ya kivita ina injini mbili na inaweza kuendeshwa kwa kasi kubwa sana na ni ndege ya kivita ya kizazi cha nne.

Inaaminika kuwa Kituo Maalumu cha Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Isfahan katikati mwa Irani kitakuwa makao ya ndege hizo zitakazoingia Iran hivi karibuni.

Shirika la Umoja wa Ndege la Urusi (UAC) linasema ndege ya kivita ya Sukhoi Su-35 “inachanganya sifa za uwezo wa kisasa wa kivita, ni ndege yenye uwezo wa kusheheni silaha nyingi, ina mfumo wa kisasa wa vita vya kielektroniki, haiyonekani kirahisi katika rada ya adui na ina uwezo wa kusalia angani muda mrefu ikiwa vitani. Wataalamu wengi wa masuala ya ulinzi wanaamini kuwa ndege ya kivita ya Russia ya Sukhoi Su-35 kwa ujumla ni bora kuliko ya Marekani ya F-35.

Iran haijanunua ndege yoyote mpya ya kivita katika miaka ya hivi karibuni, ukiondoa ndege chache za Kirusi za MiG-29 Fulcrum ilizonunua miaka ya 1990.

Kando na MiG-29, Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hutumia zaidi ndege za F-4 Phantom II, F-14 Tomcat, na F-5E/F Tiger II ambazo imejikarabatia kikamilifu kwani zilinunuliwa miaka ya 1970 wakati wa utawala wa kifalme wa kiimla  uliopinduliwa wa Pahlavi ulioungwa mkono na Marekani. Baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 Marekani ilikataa kuiuzia Iran vipuri vya ndege hizo hasa wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran lakini sasa Iran imeweza kufanikiwa kuzikarabati na zinaendesha shughuli za ulinzi wa anga ya nchi. Aidha Iran yenywe imejiundia ndege kadhaa za kivita kama vile Kowsar, Saegheh na Azarakhsh.

Iran na Russia zimetia saini mikataba mikubwa katika miezi ya hivi karibuni ili kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi, kibiashara, nishati na kijeshi.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *