Russia: Madai ya New York kuhusu milipuko ya Nord Stream ni upotoshaji

Russia imetangaza kuwa madai yaliyotolewa na gazeti la New York Times kuhusu milipuko iliyotokea kwenye mabomba ya kusafirisha gesi ya Nord Stream ni ya kubuniwa na opotoshaji wa makusudi unaofanywa na wale wanaopinga uchunguzi wa kisheria kuhusu shambulio hilo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameyasema hayo baada ya gazeti la “New York Times” kunukuu kile kilichodaiwa ni data mpya za kijasusi za Marekani kuhusu mlipuko wa mabomba ya kusafirisha gesi ya Nord Stream, na kudai kuwa hujuma hiyo ilitekelezwa na “kundi linaloiunga mkono serikali ya Ukraine”.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, ametangaza katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kwamba: “Nanajiuliza ni nani aliyeeneza habari hizi na kuziijaza kwenye vyombo vyao vya habari? Jibu ni kwamba: Ni wale ambao hawataki uchunguzi wa kisheria ufanyike na wanakusudia kupotosha watu kuhusuiana na ukweli wa mambo kwa kutumia kila njia inayowezekana.”

Zakharova amesisitiza kuwa serikali za nchi za Magharibi zilizohusika katika hujuma hiyo zinapaswa kujibu waraka rasmi uliotolewa na Russia na kuzingatia yaliyomo katika uchunguzi wa “Seymour Hersh”, mwandishi wa habari wa Marekani, na si kupindisha suala hili kwa hadithi za uwongo.

Tarehe 27 Septemba, 2022, kuliripotiwa uharibifu mkubwa kwenye mabomba ya Nord Stream, na wataalamu wa matetemeko ya ardhi wa Uswidi walirekodi milipuko miwili mnamo Septemba 26 kando ya njia za mabomba hayo. Kulipuliwa kwa mabomba ya Nord Stream 1 na 2 kulishusha chini usafirishaji wa gesi na kuvuja kwa bidhaa hiyo katika Bahari ya Baltic.

Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya amesema kuwa milipuko iliyotokea kwenye mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 ni ugaidi wa kimataifa.

Mnamo siku ya Jumatano ya tarehe 8 Februari, ripota mchunguzi wa Marekani, Seymour Hersh, alitoa ripoti yake ya uchunguzi aliofanya, akiishutumu serikali ya Washington kuwa ndiyo iliyohusika na miripuko iliyotokea Septemba mwaka jana kwenye mabomba ya usafirishaji gesi ya Nord Stream.

Kulingana na chanzo cha habari cha kuaminika kilichozungumza na Hersh, mada za miripuko ziliwekwa kwenye mabomba makuu katika Bahari ya Baltic mnamo Juni 2022 na wazamiaji wa Jeshi la Marekani kwa kutumia kivuli cha mazoezi ya kijeshi ya shirika la kijeshi NATO na kisha yakaripuliwa baadaye kwa kutumia rimoti kutokea mbali.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *