Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imelaani vikali shambulio la anga lililofanywa hivi karibuni na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria.
Siku ya Jumamosi, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia kitongoji cha Hamidiyah kusini mwa mkoa wa Tartus. Raia wawili walijeruhiwa katika shambulio hilo.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Russia imelaani shambulio hilo dhidi ya Syria na kueleza bayana kuwa kwa vyovyote vile halikubaliki.
Wizara ya mambo ya nje ya Russia imefafanua kuwa mashambulio inayofanya Israel katika ardhi ya Syria yanakiuka haki ya kujitawala nchi hiyo na kukiuka misingi mikuu ya sheria za kimataifa na ikatilia mkazo kusitishwa uvamizi huo unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Syria.
Utawala haramu wa Kizayuni umekuwa ukizishambulia kila mara ngome za jeshi la Syria na miundomsingi ya nchi hiyo kwa lengo la kutoa msukumo na uungaji mkono kwa magaidi wanaopigana na serikali halali ya Damascus.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makubwa ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi wa eneo kwa manufaa ya utawala haramu wa Israel.
Kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa Russia, jeshi la Syria limefanikiwa kulifunga faili la genge la kigaidi la DAESH (ISIS) katika nchi hiyo. Makundi mengine ya kigaidi, nayo pia yanaendelea kusambaratishwa.
Israel ina hofu na wasiwasi mkubwa wa kutokomezwa kikamilifu makundi hayo.